Hospitali ya kisasa kunufaisha wakazi Arumeru Magharibi

ARUSHA: WAKAZI wa Jimbo la Arumeru Magharibi mkoani Arusha wanatarajiwa kunufaika na ujenzi wa hospitali ya kisasa, ambao ni sehemu ya uwekezaji wenye thamani ya Sh bilioni 116 unaolenga kuboresha huduma za kijamii na kuchochea shughuli za kiuchumi katika eneo hilo.

Uwekezaji huo pia unahusisha ujenzi wa Soko la kisasa la Mateves, hoteli za nyota nne na tano pamoja na zaidi ya nyumba 94 za kupangisha zenye hadhi ya kimataifa.

Akizungumza wakati wa hafla ya kutambulisha wawekezaji katika Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Mbunge wa Arumeru Magharibi, Dk Johannes Lukumay, alisema miradi hiyo ikitekelezwa itawasaidia wananchi kupata huduma bora huku ikifungua fursa za ajira na shughuli za kiuchumi.

Alisema wawekezaji hao wako tayari kuanza utekelezaji wa miradi mara baada ya kukamilika kwa nyaraka zinazohitajika, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika kuharakisha miradi ya maendeleo.

“Nawashukuru wawekezaji hawa kwa kuonyesha nia ya kuwekeza katika Jimbo la Arumeru Magharibi. Wako tayari kuanza haraka iwezekanavyo mara nyaraka za miradi zitakapokamilika,” alisema.

Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Neema Lugangira, alimpongeza Lukumay kwa juhudi za kuvutia wawekezaji, akisema ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi utasaidia kuleta mitaji na utaalamu unaohitajika kutekeleza miradi hiyo.

Pia alimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Suleiman Msumi, kwa kuweka mazingira yanayowezesha majadiliano na wawekezaji kwa ajili ya kuleta maendeleo katika eneo hilo.

Akizungumzia uwekezaji huo, mwakilishi wa taasisi za fedha zinazofadhili miradi ya maendeleo barani Afrika kupitia mfumo wa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP), Mohamed Mazrui, alisema yuko tayari kushirikiana na halmashauri kutafuta wawekezaji na taasisi za fedha zitakazowezesha miradi hiyo.

Mazrui, anayewakilisha taasisi za Amadeus na Sahara Group of Companies, alisema taasisi hizo zina uzoefu wa kuwekeza katika nchi mbalimbali za Afrika na ziko tayari kutathmini fursa zilizopo Arumeru.

Kwa upande wake, Msumi alisema halmashauri inaendelea kutafuta wawekezaji kwa ajili ya miradi mitatu ya kimkakati, ambayo ni Soko la kisasa la Mateves, hoteli ya nyota tano katika eneo la Sekei na ujenzi wa zaidi ya nyumba 94 za kupangisha karibu na makao makuu ya halmashauri.

Alisema Soko la Mateves linatarajiwa kujengwa kwa viwango vya kimataifa, likiwa na vyumba maalumu vya baridi kwa ajili ya kuhifadhi mbogamboga, nyama na bidhaa nyingine, hatua itakayosaidia wafanyabiashara na sekta ya utalii.

Kuhusu hoteli ya nyota tano, Msumi alisema eneo la Sekei lina nafasi nzuri ya uwekezaji kutokana na ukaribu wake na Barabara ya Arusha–Moshi pamoja na makao makuu ya halmashauri.

Alisema utekelezaji wa miradi hiyo utasaidia kuongeza ajira, kukuza shughuli za kiuchumi na kupanua wigo wa mapato ya ndani ya halmashauri, ambayo inalenga kufikia zaidi ya Sh bilioni 60.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button