Wanamichezo wa bandari wamuenzi Mwalimu Nyerere

MOROGORO: WANAMICHEZO wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na Shirika la Bandari Zanzibar (ZPC) wameenzi kumbukumbu ya miaka 27 ya kifo cha Hayati Mwalimu  Nyerere kwa kushiriki fainali za michezo ya jadi, ikiwemo mchezo wa bao alioupenda.

Fainali hizo zimefanyika Oktoba 14, 2026, katika viwanja vya Bwalo la Umwema, mkoani Morogoro, ikiwa ni sehemu ya Mashindano ya 19 ya Bandari yanayotarajiwa kuhitimishwa Oktoba 15, mwaka huu.

Katika mchezo wa bao kwa wanawake, Cartace Ngajiro kutoka Bandari ya Tanga aliibuka mshindi wa kwanza baada ya kuwashinda washindani wake kutoka Bandari za Mtwara na Dar es Salaam.

Ngajiro, ambaye ni Ofisa Msaidizi wa Uhusiano wa Bandari ya Tanga, amesema ushindi huo ni sehemu ya kuenzi mchango wa wazee walioasisi na kuendeleza michezo ya jadi, hususan mchezo wa bao.

Amesema ushindi wake una maana ya pekee kwa kuwa bao lilikuwa miongoni mwa michezo aliyopenda kuucheza Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, pamoja na Rais wa kwanza wa Zanzibar, Hayati Abeid Amani Karume.

“Michezo ya jadi imeanza kuchezwa tangu enzi na enzi. Kwa kuzingatia kuwa leo ni siku ya kumbukumbu ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, ambaye mchezo wa bao ulikuwa mchezo wake pendwa, ushindi huu naukabidhi kwake kwa ajili ya kuendeleza mchezo huu,” amesema Ngajiro.

Kwa upande wa wanaume, James Mandawa kutoka Bandari za Maziwa (Lake Ports) aliibuka mshindi wa kwanza katika mchezo wa bao baada ya kuwashinda washindani wake kutoka Bandari za Dar es Salaam na Mtwara.

Mandawa amesema ushindani katika mchezo huo ulikuwa mkubwa, lakini aliweza kufanya vizuri na kuibuka mshindi wa kwanza.

Naye Nezia Daudi kutoka Bandari ya Dar es Salaam, aliyeshika nafasi ya tatu katika mchezo wa bao kwa wanawake, amesema pia ameshiriki mchezo wa drafti na kufanikiwa kutwaa ushindi wa kwanza kwa mchezo huo ambao mwaka uliopita ulishikiliwa na mwenzake ambaye amestaafu.

Matokeo ya michezo mingine

Katika mchezo wa drafti kwa wanawake, Bandari ya Dar es Salaam ilitwaa ubingwa, ikifuatiwa na Bandari ya Tanga katika nafasi ya pili, huku Bandari ya Mtwara ikishika nafasi ya tatu.

Kwa upande wa wanaume, Bandari ya Tanga ilitwaa nafasi ya kwanza, Bandari ya Mtwara ikishika nafasi ya pili, huku Lake Ports ikimaliza katika nafasi ya tatu.

Katika mchezo wa karata kwa wanawake, Bandari ya Dar es Salaam ilitwaa ushindi wa kwanza, ikifuatiwa na Lake Ports katika nafasi ya pili, huku TPA Makao Makuu ikishika nafasi ya tatu.

Kwa wanaume, Bandari Zanzibar ilitwaa ushindi wa kwanza, Bandari ya Dar es Salaam ikishika nafasi ya pili, huku TPA Makao Makuu ikimaliza katika nafasi ya tatu.

Mashindano hayo ni sehemu ya shughuli za kuimarisha mshikamano miongoni mwa wanamichezo wa taasisi za bandari, huku yakitoa nafasi ya kuendeleza michezo ya jadi na kuhifadhi urithi wa kitamaduni.

Habari Zifananazo

One Comment

  1. Excellent blog! Do you have any helpful hints for aspiring writers?

    I’m hoping to start my own blog soon but I’m a little lost on everything.
    Would you recommend starting with a free platform like WordPress or go for a paid option? There are so
    many options out there that I’m completely confused ..
    Any ideas? Many thanks!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button