JKCI, AU kushirikiana tiba magonjwa yasiyoambukiza

DAR ES SALAAM; Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), imesaini Hati ya Makubaliano (MoU) na Tume ya Umoja wa Afrika (AU) kwa ajili ya kuhudumia na kuwapatia matibabu ya magonjwa ya moyo pamoja na magonjwa mengine yasiyoambukiza kwa wafanyakazi wa umoja huo.
Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk Peter Kisenge alisema makubalino hayo yanaifanya JKCI kuwa mshirika rasmi wa kutoa huduma za afya kwa Tume ya Umoja wa Afrika.
Amesema hayo wakati wa hafla fupi ya kusaini hati ya makubaliano ya ushirikiano katika kutoa huduma ya magonjwa ya moyo kwa wafanyakazi wa wa umoja wa Afrika yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Kisenge amesema makubalinao haya yametokana na juhudi kubwa za uwekezaji wa vifaa tiba, wataalamu na miundombinu rafiki ambayo imetengenezwa kwa lengo la kutoa huduma bora na za kibingwa za moyo nchini.
“Kusaini huku kwa MoU hakujaja tu kumekuja kutokana na uwekezaji mkubwa ambao umefanywa na serikali yetu ya awamu ya sita ikiongozwa na Dk Samia hasa katika vifaa tiba vile vile rasilimali watu,”alisema Kisenge
Ameongeza kuwa JKCI imekuwa ikihudumia wananchi kutoka nchi zaidi ya 20 za Afrika zinazofuata huduma za tiba na upasuaji wa moyo nchini Tanzania, hii ni kutokana na mafanikio ya mpango wa Tiba Mkoba wa Dk Samia ambao umevuka mipaka na kwenda kutoa huduma barani Afrika.

” Zaidi ya wagonjwa 3,000 nchini Comoro, wagonjwa 756 nchini Malawi, Zambia walihudumiwa zaidi ya wagonjwa 50 ambapo watoto walifanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo,”amesema na kuongeza:
“Nia ya JKCI ni kuhakikisha kwamba Waafrika wanapata huduma bora ya moyo na sisi JKCI tunataka kuhakikisha Afrika yote inapata huduma kwa magonjwa ya moyo”
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za tiba kutoka Tume ya Umoja wa Afrika, Dk Adamu Isah alisema makubalinao haya yalifikiwa kutokana na kuridhishwa na viwango vya utowaji huduma na wataalamu waliopo katika Taasisi hiyo.
“Tuliwahi kufika hapa mwaka mmoja uliopita tumeona ubora wa huduma wataalamu walio nao, vifaa tiba, na uwezo wa kupima magonjwa na tuliona wametimiza viwango vyote tunavyohitaji ili kuhudumia wagonjwa weto,”alisema Dk Isah.

Amefafanua kuwa Tanzania ni mwanachama muhimu sana wa Umoja wa Afrika, na kwamba wanajisikia nyumbani na wana amani kuwa wafanyakazi wao watapata huduma bora.
“JKCI itaweza kusaidia misheni za Umoja wa Afrika, mikutano, na mikutano mikuu ya wakuu wa nchi itakayofanyika hapa,” alisema.
Aidha alipongeza kwa ushirikano alioupata tangu umoja wa afrika ulipoanza mazungumzo na taasisi ya JKCI hadi kufikia mafanikio.



