TBS yataka wazalishaji bidhaa za chakula wazingatie viwango

TANGA; Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limetaka wazalishaji wa bidhaa za chakula nchini kuzingatia viwango na ubora katika uzalishaji, ili kulinda afya na usalama wa watumiaji, pamoja na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani, kikanda na kimataifa.
Wito huo umetolewa na Mhandisi Cyril Kimario, Kaimu Meneja wa TBS Kanda ya Mashariki, wakati wa Maonesho ya Siku ya Chakula Duniani yaliyofanyika katika Viwanja vya Usagara, mkoani Tanga.
Amesema maonesho hayo yamekuwa fursa muhimu kwa TBS kukutana na wadau na wazalishaji wa bidhaa za chakula, kuwapatia elimu na kuwaelekeza kuhusu umuhimu wa kuzingatia viwango katika hatua mbalimbali za uzalishaji ili kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa ni bora na salama kwa matumizi ya walaji.
Ameeleza kuwa, kwa mujibu wa matakwa ya sheria, wazalishaji wa bidhaa za chakula wanapaswa kuhakikisha bidhaa zao zinakidhi matakwa ya viwango vinavyotumika kabla ya kuziingiza sokoni.
Hatua hiyo inalenga kuwalinda watumiaji dhidi ya madhara yanayoweza kusababishwa na matumizi ya bidhaa zisizokidhi matakwa ya viwango.

“Sheria ya Viwango inamtaka mzalishaji wa bidhaa za chakula kuhakikisha anazalisha bidhaa bora na salama. Bidhaa za chakula zisizokidhi viwango zinaweza kusababisha madhara kwa afya ya walaji na kuathiri nguvu kazi ya Taifa,” amesema Kimario.
Aidha, ameeleza kuwa Serikali imeweka utaratibu wa kuwawezesha wajasiriamali wadogo na wa kati kupata huduma za uthibitishaji wa ubora wa bidhaa bila malipo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwaunga mkono katika kuzalisha bidhaa bora na salama.
“TBS inawaasa wajasiriamali wadogo wanaozalisha bidhaa za chakula kutumia fursa hii kwa kutembelea ofisi za Shirika ili kupata maelekezo na huduma za uthibitishaji wa ubora wa bidhaa zao,” amesisitiza Mhandidsi Kimario.

Akizungumzia huduma za upimaji, amesema maabara za TBS zinafanya kazi kwa kuzingatia matakwa ya umahiri wa kimataifa, jambo linalochangia kuhakikisha matokeo ya vipimo yanakuwa ya kuaminika na kukubalika kwa mujibu wa taratibu na makubaliano husika.
Ameongeza kuwa TBS ina ofisi katika kanda mbalimbali nchini zinazotoa huduma na elimu kuhusu viwango na ubora wa bidhaa, hivyo, amewahimiza wajasiriamali kuendelea kutembelea ofisi hizo hata baada ya kumalizika kwa maonesho hayo ili kupata ushauri, mwongozo na taarifa kuhusu huduma zinazotolewa na Shirika.

Akizungumzia kaulimbiu ya maadhimisho hayo isemayo Ubunifu wa Leo, Lishe Bora ya Kesho Kuelekea Dira 2050, Mhandisi Kimario amesema TBS itaendelea kutekeleza jukumu lake la kuwaelimisha wazalishaji kuhusu umuhimu wa kuzingatia viwango, ubora na usalama wa bidhaa za chakula, kwa lengo la kulinda afya za walaji na kukuza ushindani wa bidhaa zinazozalishwa nchini.




Thanks in favor of sharing such a nice thinking, paragraph is
pleasant, thats why i have read it completely