Wafanyabiashara wa Tanzanite wahimizwa kuwekeza elimu

ARUSHA: WAFANYABIASHARA wa madini ya Tanzanite katika Mji wa Mirerani, Wilaya ya Simanjiro, Mkoa wa Manyara, wamehimizwa kuwekeza katika elimu kwa lengo la kuimarisha mustakabali wa watoto na kuchangia maendeleo ya jamii, wakitakiwa kuiga mfano wa mfanyabiashara Justin Nyari.

Wito huo umetolewa na wajumbe wa Kamati ya Maendeleo ya Kata ya Endiamtu wakiongozwa na Diwani wa kata hiyo, Lucas Zacharia, pamoja na Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mirerani, Hans Nkya, walipotembelea Shule ya Glisten Pre & Primary School inayomilikiwa na Nyari, kabla ya mahafali yake ya sita.

Zacharia amesema iwapo wafanyabiashara wengi wa Tanzanite wangewekeza katika maendeleo ya jamii kama anavyofanya Nyari, Mirerani ingepiga hatua kubwa katika maendeleo.

“Hapa Mirerani tungekuwa na wadau 10 wa maendeleo kama Nyari, tungepiga hatua kubwa mno ya maendeleo kwa namna ambavyo amekuwa akijitoa kwa jamii,” amesema Zacharia.

Kwa upande wake, Nkya, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kisimani kilipo shule hiyo, amesema Glisten imekuwa ikiipa sifa eneo hilo, wilaya na mkoa kutokana na kufanya vizuri katika mitihani ya kitaifa.

“Glisten Pre & Primary School ipo kwenye eneo letu na inatoa sifa kubwa kwetu kutokana na taaluma inayotoa, kwani ufaulu wake mara nyingi ni wa kitaifa na tunapata pongezi nyingi,” amesema Nkya.

Naye Mwenyekiti mstaafu wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mirerani, Adam Kobelo, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Zaire, amesema Nyari ni miongoni mwa watu wanaoipenda Mirerani na kuwataka wachimbaji pamoja na wafanyabiashara wengine kuiga mfano wake kwa kuwekeza katika eneo hilo badala ya kuelekeza uwekezaji wao katika maeneo mengine ya nchi.

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Denis Costantin, amewashukuru wajumbe wa Kamati ya Maendeleo ya Kata ya Endiamtu kwa kuwatembelea na kuungana nao katika kipindi cha kuelekea mahafali ya sita ya shule hiyo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button