Kiruswa akabidhi vifaa shule ya Lesing’ita

LONGIDO: NAIBU Waziri wa Madini na Mbunge wa Jimbo la Longido mkoani Arusha, Dk. Stephen Kiruswa, amekabidhi mashine ya kunakili na kuchapisha nyaraka pamoja na kompyuta kwa Shule ya Msingi Lesing’ita, vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni tatu, ili kupunguza gharama za shule katika uchapishaji wa karatasi za mazoezi, mitihani na shughuli nyingine za kitaaluma.
Sambamba na msaada huo, Kiruswa ameahidi kushirikiana na marafiki zake kujenga madarasa mawili na nyumba ya mwalimu kwa shule hiyo iliyopo Kata ya Mundarara, Wilaya ya Longido.
Amemwagiza Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Jackline Bendera, kumpatia haraka ramani za majengo hayo ili kuwezesha kuanza kwa ujenzi.

Kiruswa alitoa ahadi hizo katika kikao cha ndani kilichowakutanisha kamati ya uongozi wa shule, walimu pamoja na viongozi wa kijiji na kata, akieleza kuwa msaada wa vifaa hivyo ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa mwaka jana wakati wa kampeni.
Alisema shule hiyo imekuwa ikipiga hatua za maendeleo mwaka hadi mwaka, hivyo changamoto zinazokabili uendeshaji wake zinahitaji kushughulikiwa ili kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji.
Alizitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na upungufu wa walimu, madarasa, nyumba za walimu na kivuko cha kufikia shule hiyo, akisema atazifanyia kazi kwa kuwa anaamini ziko ndani ya uwezo wake.
Alisisitiza kuwa upatikanaji wa vifaa vya kuchapisha utasaidia kupunguza gharama ambazo shule imekuwa ikitumia kupata huduma hizo nje ya shule.

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Lesing’ita, Jackline Bendera, alimshukuru Kiruswa kwa msaada huo, akisema umefika wakati muafaka na utasaidia kurahisisha shughuli za kila siku za shule. Aliwaomba wadau wengine wa maendeleo kujitokeza kuisaidia shule hiyo ili kukabiliana na changamoto zilizopo.
Bendera alisema shule inakabiliwa na uhaba wa walimu, hali inayowalazimu walimu waliopo kufundisha masomo mengi. Aliomba changamoto hiyo ishughulikiwe haraka, ikiwemo kuangaliwa kwa suala la ajira kwa walimu wa mazoezi. Aliongeza kuwa upungufu wa madarasa na nyumba za walimu ni miongoni mwa changamoto kubwa zinazohitaji msaada.

Naye Diwani wa Kata ya Mundarara, Alais Mushao, alisema Shule ya Msingi Lesing’ita imekuwa ikifanya vizuri mwaka hadi mwaka, hivyo inahitaji kuungwa mkono ili kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuwapa walimu motisha ya kuendelea kufanya vizuri katika ufundishaji wa wanafunzi.



