‘Leseni utafutaji mafuta, gesi zitaipaisha TPDC ‘

DAR ES SALAAM: Serikali imesema utoaji wa leseni nne za utafutaji wa gesi asilia kwa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) utaimarisha uwezo wa shirika hilo katika kusimamia na kuendeleza rasilimali za mafuta na gesi, kuongeza upatikanaji wa nishati na kuchochea maendeleo ya viwanda nchini.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini wa leseni hizo zilizofanyika jijini Dar es Salaam, Makamu wa Rais Deogratius Ndejembi amesema hatua hiyo inalenga kuiwezesha TPDC kushiriki kikamilifu katika mnyororo mzima wa thamani wa sekta ya mafuta na gesi, badala ya kutegemea zaidi nafasi ya mshirika mdogo katika miradi ya utafutaji na uzalishaji wa rasilimali hizo.
Ndejembi ameeleza kuwa Tanzania ilianza kutafuta mafuta katika miaka ya 1970, lakini utafiti uliofanyika katika maeneo ya Mnazi Bay na Songo Songo ulisaidia kubaini uwepo wa gesi asilia.
Amesema Matumizi ya rasilimali hiyo yalipanuka baadaye, hasa katika uzalishaji wa umeme, huku miundombinu ya gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam ikichangia kuongeza upatikanaji wa nishati na kupunguza utegemezi wa vyanzo vya maji wakati wa ukame.
Aidha, amesema matumizi ya gesi asilia kwa sasa yamepanuka zaidi ya uzalishaji wa umeme, yakijumuisha matumizi ya majumbani, magari kupitia mfumo wa gesi asilia iliyoshindiliwa (CNG), na shughuli za viwanda, huku akibainisha kuwa rasilimali hiyo pia ina nafasi ya kusaidia uzalishaji wa mbolea na kemikali za viwandani.

Ndejembi pia amesisitiza kuwa TPDC inapaswa kuimarisha uwezo wa wataalamu wazawa, usimamizi wa miradi na matumizi bora ya mitaji, huku ikihakikisha shughuli zote zinafanyika kwa kuzingatia sheria, masharti ya leseni, viwango vya usalama na utunzaji wa mazingira.
Aliongeza kuwa ushirikiano na wawekezaji wenye uwezo wa kifedha na kiteknolojia ni muhimu kutokana na gharama kubwa za utafutaji wa gesi asilia.
Hata hivyo, Ndejembi ametoa wito kwa TPDC na wadau wa sekta hiyo kuhakikisha jamii zinazozunguka maeneo ya miradi zinanufaika na uwekezaji kupitia huduma za kijamii, ikiwemo elimu na afya



