Miradi ya tril 8/- ipo kwenye utekelezaji

DAR ES SALAAM: Serikali imetangaza jumla ya miradi 10 inayotekelezwa kwa mfumo wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) ilikuwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2026/27.
Miradi hiyo ina jumla ya mtaji wa Sh trilioni 8.6, jambo linaloonyesha jinsi Serikali inavyoitegemea sekta binafsi katika kuleta maendeleo makubwa ya miundombinu bila kutegemea fedha za Bajeti peke yake.
Miongoni mwa miradi hiyo mikubwa ni Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT), Awamu ya Kwanza na ya Pili, ambao unalenga kuboresha usafiri wa mijini jijini Dar es Salaam.
Mradi huu unatarajiwa kupunguza msongamano wa magari, kuokoa muda wa wananchi na kuongeza ufanisi wa usafirishaji. Pia unatoa fursa kwa wawekezaji binafsi kuwekeza kwenye mabasi ya kisasa, vituo na mifumo ya tiketi za kidijitali.
Mradi mwingine ni Ujenzi na Uendeshaji wa Jengo la Biashara la DDC Kariakoo, ambalo linatarajiwa kuwa kitovu cha biashara katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
Kupitia mfumo wa PPP, mwekezaji binafsi anajenga na kuendesha jengo hilo kwa kipindi fulani, huku Serikali ikipata mapato kupitia kodi na gawio. Hii ni mfano wa jinsi PPP inavyoweza kutumika kukuza biashara za ndani na kuongeza ajira kwa vijana.
Orodha ya miradi hiyo pia inajumuisha uanzishwaji wa vituo vya ukaguzi wa lazima wa vyombo vya moto, uboreshaji wa uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam, pamoja na ukarabati na uendeshaji wa Reli ya TAZARA.
Bandari ya Dar es Salaam ni lango kuu la biashara kwa Tanzania na nchi jirani, hivyo kuboreshwa kwake kutasaidia kuongeza kasi ya kupakua na kupakia mizigo. Vivyo hivyo, TAZARA ni muhimu kwa usafirishaji wa shehena kati ya Tanzania na Zambia.
Mwisho, mradi wa ujenzi wa kituo cha kisasa cha huduma za usafirishaji shehena chini ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) pia upo kwenye orodha hiyo.
Kituo hiki kitasaidia kuboresha mnyororo wa usafirishaji wa mizigo nchini. Kwa ujumla, miradi hii 10 inaonyesha kuwa Serikali inaamini kuwa PPP ni njia sahihi ya kutatua changamoto ya uhaba wa fedha za miradi mikubwa ya maendeleo.



