Mchengerwa: Rejesheni matumaini kwa wagonjwa

DAR ES SALAAM; Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, amewataka wahudumu wa afya nchini kuwahudumia wagonjwa kwa lugha nzuri, upole, heshima na upendo ili kurejesha matumaini kwa wagonjwa wanaofika hospitalini hapo kutafuta matibabu.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati alipofanya ziara katika Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila amesema kila mgonjwa anayefika hospitalini anapaswa kupokelewa vizuri na kuhudumiwa kwa haraka, akisisitiza kuwa jukumu la watumishi wa afya si kutoa matibabu pekee, bali pia kuwapa wagonjwa matumaini ya kuendelea kuishi.

“Wagonjwa wanafika hospitalini wakiwa katika hali mbaya au wamekata tamaa wanahitaji kuhudumiwa kwa weledi na upendo, ili kurejesha hali zao na kuwafanya wawe na matumaini ya kupona,” amesema.

Aidha amewapongeza viongozi na watumishi kwa kuboresha huduma, akieleza kuwa malalamiko yaliyokuwa yakitolewa na wananchi kupitia mitandao ya kijamii yamepungua.

Amepongeza Mkurugenzi na Mkurugenzi Msaidizi kwa kutekeleza maelekezo aliyoyatoa katika ziara iliyopita, hatua ambayo amesema imeongeza kasi ya utendaji na kuboresha huduma zinazotolewa kwa wagonjwa.

“Mloganzila ni taasisi kubwa inayojumuisha huduma za matibabu na mafunzo, hivyo uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika miundombinu yake unapaswa kuendana na ubora wa huduma zinazotolewa,”amesisitiza.

Amesema hospitali hiyo inapokea wagonjwa wenye changamoto mbalimbali za kiafya, wakiwemo wagonjwa mahututi, wenye saratani, kiharusi na wanaohitaji huduma za usafishaji damu kutokana na matatizo ya figo.

Aidha, ameeleza kuwa amepata taarifa za kupungua kwa kiwango cha vifo vya wagonjwa na kufikia kiwango kinachokubalika kimataifa, huku akiwataka watumishi kuendeleza mafanikio hayo.

Amewataka kutokukatishwa tamaa na changamoto au malalamiko yanayotolewa mitandaoni, badala yake waendelee kutekeleza majukumu yao kwa bidii na kuhakikisha kila mgonjwa anayefika hospitalini hapo anapata huduma kwa wakati.

Amesema ana imani na uwezo wa hospitali hiyo kutokana na uwepo wa madaktari bingwa, madaktari bingwa bobezi na wataalamu wengine, akisisitiza kuwa Mloganzila inapaswa kuwa sehemu ya matumaini kwa kila Mtanzania anayehitaji huduma za afya.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button