Viwanda vya dawa Mloganzila kuanza uzalishaji Mei 2027

DAR ES SALAAM; Wawekezaji wamejitokeza kuwekeza katika Kongani ya Viwanda ya Mloganzila, Dar es Salaam, huku ujenzi wa viwanda vya bidhaa tiba ukipiga hatua na uzalishaji wa baadhi ya vifaa tiba ukitarajiwa kuanza Mei 2027.
Kikosi Kazi cha Kitaifa cha Kuharakisha Uwekezaji katika Viwanda vya Bidhaa Tiba (PIAT) kimeridhishwa na hatua iliyofikiwa katika uanzishaji wa viwanda hivyo, kufuatia ziara ya kikosi hicho iliyofanyika jijini Dar es Salaam ikiongozwa na Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mchengerwa amesema Serikali imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji katika sekta ya bidhaa tiba, hivyo amewataka wawekezaji kutumia fursa hiyo kuanzisha viwanda nchini ili kuongeza uzalishaji wa bidhaa zinazohitajika katika huduma za afya.
Amesema uwekezaji huo una umuhimu mkubwa katika kupunguza utegemezi wa bidhaa tiba kutoka nje ya nchi, kuongeza upatikanaji wa vifaa tiba na kukuza uchumi kupitia uzalishaji wa ndani.
Mchengerwa amesisitiza kuwa wawekezaji wana uhakika wa soko la bidhaa tiba siyo Tanzania pekee, bali pia katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na ukanda wa Kusini mwa Afrika, hivyo kuwataka kuongeza kasi ya utekelezaji wa mipango yao ya uwekezaji.
“Serikali itaendelea kushirikiana na wawekezaji kuhakikisha changamoto zinazoweza kuchelewesha uanzishaji wa viwanda hivyo zinapatiwa ufumbuzi ili kufikia malengo yaliyowekwa.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya anayeshughulikia mambo ya dawa, Emmanuel Tayari, amesema eneo lote la Kongani ya Viwanda ya Mloganzila tayari limepata wawekezaji ambao wamewasilisha mipango kazi yao kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa miradi hiyo.

Amesema miongoni mwa wawekezaji waliopo ni Kampuni ya Hongyu, ambayo inaendelea kukamilisha ujenzi wa majengo yatakayotumika kuanzisha viwanda vya vifaa tiba nchini.
Tayari amesema kampuni hiyo ina uwezo mkubwa wa kuzalisha na kuuza vifaa tiba katika soko la Ulaya, jambo linaloonesha fursa iliyopo kwa Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji na usambazaji wa bidhaa tiba katika masoko ya kimataifa.
Ameeleza kuwa matunda ya uwekezaji huo yanatarajiwa kuanza kuonekana kuanzia Mei 2027, ambapo uzalishaji wa takribani asilimia 60 ya vifaa tiba unatarajiwa kuanza, hatua itakayochangia upatikanaji wa bidhaa hizo ndani ya nchi.

Kongani ya Viwanda ya Mloganzila iliyopo Wilaya ya Ubungo, Dar es Salaam, ilizinduliwa Mei 8, 2026, ikiwa na ukubwa wa takribani ekari 450 kwa ajili ya kuvutia uwekezaji katika uzalishaji wa bidhaa mbalimbali za tiba.
Kikosi Kazi cha PIAT kinaundwa na wataalamu kutoka sekta za afya, viwanda na uwekezaji chini ya usimamizi wa Wizara ya Afya, kikiwa na jukumu la kuratibu na kuharakisha uwekezaji katika viwanda vya bidhaa tiba nchini ili kupunguza uagizaji wa bidhaa hizo kutoka nje na kuimarisha sekta ya afya.



