Dar City kuibeba Tanzania mashindano Afrika

DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, ameitaka timu ya Dar City kwenda kupambana na kutetea heshima ya Tanzania katika mashindano ya mpira wa kikapu ya Afrika yatakayofanyika Nairobi, Kenya.

Makonda ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kuiaga na kuikabidhi bendera ya Taifa timu hiyo, akisisitiza kuwa safari ya Dar City si ya klabu pekee bali ni uwakilishi wa nchi nzima.

“Dar City imebeba heshima ya basketball ya Taifa. Tunawatuma si kama klabu au timu ya mtu binafsi, tunawatuma kama nchi,” amesema Makonda.

Amesema timu hiyo ina dhamana ya kupeperusha bendera ya Tanzania na kufungua milango kwa klabu nyingine za kikapu nchini kuona kuwa zinaweza kushiriki na kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.

Amesisitiza kuwa anatarajia Dar City kufanya vizuri na kupata ushindi katika michezo yake ili kusonga mbele katika hatua zinazofuata za mashindano hayo, akiwataka wachezaji kulitambua jukumu walilopewa.

Katika hatua nyingine, Makonda amezitaka kampuni, taasisi na wadau mbalimbali kuwekeza katika mpira wa kikapu kwa kuanzisha na kudhamini timu nyingi zaidi ili vipaji vilivyopo nchini viweze kuendelezwa na kuwa fursa za kiuchumi.

Amesema Serikali inaendelea kutekeleza mipango ya kukuza michezo nchini, ikiwemo kuboresha miundombinu na kuongeza ushiriki wa Watanzania katika michezo mbalimbali.

Ameeleza kuwa Wizara imefikia asilimia 39 ya utekelezaji wa mipango yake, ikiwa na lengo la kufikia asilimia 100 ili michezo iwe sehemu ya maisha ya Watanzania na kutoa fursa kwa vipaji kujitokeza.

Makonda pia amewashukuru mashabiki wa Dar City kwa kuendelea kuiunga mkono timu hiyo na kueleza kuwa Serikali itaangalia uwezekano wa kuwawezesha baadhi yao kwenda Nairobi kuishangilia timu wakati wa mashindano hayo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button