Teknolojia kurahisisha biashara AFCON 2027

ARUSHA: Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imeandaa mifumo mbalimbali ya kidijitali inayolenga kuwawezesha mama lishe, watoa huduma za hoteli na malazi, nyama choma pamoja na wadau wa utalii kutangaza biashara zao, kupokea oda, kurahisisha malipo na kuwafikia wateja kwa urahisi kuelekea mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.

Mifumo hiyo inalenga kuwaunganisha watoa huduma na wateja kupitia majukwaa ya kidijitali, kuongeza fursa za biashara na kukuza uchumi wa kidijitali, huku ikiwarahisishia wageni watakaotembelea Tanzania kupata huduma mbalimbali wakati wa mashindano hayo.

Akizungumza kuhusu mifumo hiyo, Mkurugenzi Msaidizi wa Anwani za Makazi katika wizara hiyo, Mhandisi Edith Turuka, amesema maandalizi hayo ni sehemu ya jukumu la wizara katika kusimamia na kuendeleza sekta ya mawasiliano na teknolojia ya habari nchini, sambamba na mageuzi ya kidijitali na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.

Amesema mifumo hiyo inajumuisha Mfumo wa Anwani za Makazi (NAPA), Jamii Apps na JamiiPay, ambayo imeandaliwa kuboresha utoaji wa huduma, kurahisisha upatikanaji wa taarifa na kuwawezesha wafanyabiashara kutumia teknolojia katika shughuli zao.

Amefafanua kuwa NAPA itasaidia kutambua maeneo kupitia namba za majengo na majina ya mitaa na barabara, hivyo kurahisisha wateja kuwafikia watoa huduma.

Kuhusu Jamii Apps, amesema ni jukwaa linalounganisha huduma mbalimbali za Serikali na sekta binafsi, wakati JamiiPay itarahisisha malipo ya kielektroniki kupitia huduma za Jamii Full, Jamii Shop na Jamii Wallet, pamoja na kusimamia bidhaa na oda za wateja.

Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi, Utawala na Rasilimali Watu wa Mkoa wa Arusha, Mosses Pesha, aliyemwakilisha Katibu Tawala wa Mkoa huo, Dk. Toba Nguvila, amesema wafanyabiashara wanapaswa kutumia fursa ya teknolojia kuboresha utoaji wa huduma na kujiandaa kuwapokea wageni watakaotembelea nchini.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button