Tulia amfagilia Rais Samia kwa maono kwenye kilimo

SPIKA wa Bunge, Dk Tulia Ackson, amesema Tanzania itailisha dunia na itatambua kuwa yanatoka Tanzania.

Pia amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa maono aliyonayo kuhusu Taifa hili na akataka uwepo ushirikiano wa wizara zote.

Ameyabainisha hayo Chinangali II mkoani Dodoma jana wakati wa uzinduzi wa mashamba makubwa ya pamoja katika programu ya ‘Building Better Tomorrow’ (BBT) uliofanywa na Rais Samia.

Dk Tulia alisema anaamini mashamba hayo ya mfano yataendelea na yatakuwa mengi zaidi, hivyo yanahitaji ushirikiano wa wizara zote.

Alisema mashamba hayo yatahitaji kumwagiliwa hivyo yanahitaji pampu za umeme, hivyo Waziri wa Nishati atapaswa kueleza namna gani jambo hilo litakuwa katika uhalisia, pia Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara naye atahusika kwa kuwa programu hiyo siyo tu kwamba itailisha Tanzania bali na dunia pia.

“Tunatamani tuilishe dunia katika mazao yale ambayo ni ya chakula, lakini kwa sababu kilimo kitahusisha pia mazao ya biashara, ni dhahiri tunahitaji viwanda ili biashara yetu Tanzania ikue, kwa hiyo tunahitaji uwekezaji zaidi,” alisema Dk Tulia.

Aliongeza: “Kwa hiyo Mheshimiwa Rais nikuombe, Wizara zako zote na ningekuwa na muda ningeeleza kila wizara ninavyoona inaweza kushiriki vipi katika haya maono yako, lakini naamini kwamba katika bajeti ijayo, hiki ambacho umekizindua leo, tunatarajia kuona muunganiko wa serikali ikiwa moja kwenye suala hili la mapinduzi ya kilimo.”

Kwa mujibu wa Dk Tulia, aliwahi kusema wakati Rais Samia anazindua ujazaji maji wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) kuwa bwawa hilo litasaidia kwenye kilimo na Tanzania italisha dunia.

Dk Tulia alisema alitoa kauli hiyo si kwa kukosea, alimaanisha Tanzania ina uwezo wa kuilisha dunia kwa mazao yake na watu watakula wakijua yametoka Tanzania.

“Mazao haya yanayozalishwa yanahitaji miundombinu bora ili yafike sokoni kwa haraka, hivyo haya yote tunapoyaweka pamoja ni dhahiri kwamba Taifa letu linapiga hatua kubwa chini ya uongozi wako,” alisema.

Dk Tulia alisema anatambua kuwa kuna watu hawawaelewi wanapompongeza Rais Samia, lakini ukweli ni kwamba Rais Samia ameleta fedha zimejenga barabara, miradi ya maji na jana alizindua BBT, hivyo hawana budi kumpongeza na kumpa sifa anazostahili kwa maono yake hayo.

Pia alimhakikishia Rais Samia kuwa Bunge litaendelea kumpa ushirikiano na kuhakikisha wanaishauri serikali sawasawa pamoja na kuisimamia kwa mambo ambayo iliahidi Watanzania.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button