SMZ yaangalia sheria kudhibiti upotevu wa fedha

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imesema itafanya marekebisho ya sheria zake kwa baadhi ya taasisi zinazosimamia sheria na utumishi wa umma ili kudhibiti ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha za serikali.

Akizungumza katika kilele cha siku ya watumishi wa umma katika ukumbi wa Sheikh Idris Abdul Wakil Unguja, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi alisema kuwepo kwa sheria madhubuti zitasaidia kusimamia na kupambana na matukio ya matumizi mabaya ya fedha za serikali pamoja na ofisi za umma kwa watendaji.

Alisema sheria za kupambana na rushwa na uhujumu wa uchumi, sheria ya Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na Tume ya maadili zitafanyiwa marekebisho kwa lengo la kuongeza ufanisi na uwajibikaji kwa watumishi wa umma.

Alisema kuwepo kwa matumizi ya mifumo ya kielektroniki katika maeneo yote ikiwemo ya watumishi wa umma kwa kiasi kikubwa utakwenda sambamba na kuziba mianya ya upotevu wa mapato pamoja na kupambana na rushwa.

Aliwataka watumishi wa umma kuongeza ufanisi katika sehemu za kazi kwa ajili ya kuyafikia malengo yake yanayokwenda sambamba na utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kwa mfano alisema serikali imefanikiwa kutengeneza muongozo kwa watumishi wa umma wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano waliopo Zanzibar ikiwa ni sehemu ya kumaliza changamoto zilizokuwa zikijitokeza wakati wa kustaafu.

Aidha, alisema serikali imefanikiwa kuzindua mfumo wa Zan Ajira ambao kazi yake kubwa kuangalia mwenendo wa ajira zote zinazotolewa na kuepuka upendeleo.

Akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene alisema amefurahishwa na utendaji unaokwenda na kasi ya mabadiliko makubwa ya kiuchumi na utoaji wa huduma za kijamii kwa wananchi.

Alipongeza mageuzi makubwa yanayofanyika sasa kutoka utumishi wa mazoea kwenda na matumizi ya mifumo ya kielektroniki ambayo kwa kiasi kikubwa yataongeza ufanisi na kupambana na rushwa.

Aidha, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Sheria, Katiba, Utumishi na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman alisema katika kipindi cha uongozi wa Dk  Mwinyi mabadiliko makubwa ya sheria na utumishi pamoja na uwajibikaji yamefanyika.

Mapema Katibu Mkuu, Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Utumishi na Utawala Bora, Mansura Mossi Kassim akizungumza alisema serikali imejipanga kuongeza kasi ya uwajibikaji ambayo ndiyo itakayoongeza mapato ya nchi.

Alisema katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa serikali ya awamu ya nane chini ya Dk Mwinyi, mafanikio makubwa yamepatikana ikiwemo kasi ya ukusanyaji mapato ambayo ni sehemu ya uwajibikaji kwa watendaji katika kufikia malengo ya utumishi uliotukuka.

Katika maadhimisho hayo, Dk Mwinyi alizindua mfumo wa Zan ajira ambao kazi yake kubwa ni kuratibu mwenendo wa ajira kwa watumishi wa umma pamoja na kuhakiki na kufuatilia maslahi yao wakati wanapostaafu.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button