WAUMINI na viongozi wa dini wa Kiislamu wakiongozwa na Sheikh wa Mkoa wa Dodoma, Alhaj Mustafa Rajabu Shaban, wamemshukuru Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde kwa ukarabati mkubwa wa Msikiti wa Masjid Salum Ally uliopo Hombolo Bwawani jijini Dodoma.
Akizungumza na waumini wa msikiti huo Sheikh Shaban amesema, Mavunde amekuwa mstari wa mbele kushirikiana na waumini wa dini ya kiislamu mkoani humo na kuwataka waumini hao kumuombea kwa Mwenyezi Mungu amjaalie baraka na amkinge na aina zote za shari kwa kuwa amefanya jambo kubwa na la kumpendeza Mungu.
Akitoa salamu za awali Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Alhaj Jabir Shekimweri amempongeza Mavunde kwa majitoleo yake na kugusa watu wote katika jamii bila ubaguzi na kuahidi kujenga jengo la madrassa kama sehemu ya kuunga mkono kazi kubwa iliyofanyika na pia kutoa shukrani kwa Mwenyezi Mungu.

Msikiti huo ulianzishwa mwaka 1954 kutokana na uchakavu mkubwa wa msikiti huo uongozi wa msikiti ulimuomba Mbunge Mavunde kuufanyia marekebisho, ambapo jumla ya sh milioni 33 zimetumika.
Aidha kwa upande wa Mavunde akizungumza na waumini hao amesema ni dhamira yake kuhakikisha anashiriki katika shughuli za maendeleo ya kijamii kwa kugusa jamii yote na kuahidi kuendelea kushirikiana na wanajamii hasa taasisi za dini katika masuala mbalimbali.

“Ninawashukuru sana uongozi wa Msikiti Masjid Salum Ally kwa imani yao kubwa kwamba ninaweza kusimamia ukarabati wa msikiti huu mkongwe, namshukuru zaidi Mungu na marafiki zangu mlioniunga mkono kukamilisha ukarabati wa ujenzi huu, ”amesema Mavunde.
Back to top button