Sh bilioni 48 zatengwa mikopo wanafunzi wa diploma

DAR ES SALAAM: SERIKALI imetenga Sh bilioni 48 kwa ajili ya kuwakopesha wanafunzi 8,000 watakaodahiliwa kusoma Stashahada (Diploma) katika fani za kipaumbele kwa mwaka wa masomo 2023/24.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda wakati wa Uzinduzi wa ‘Mwongozo wa Utoaji Mikopo ya Elimu kwa Wanafunzi wa Stashahada’ leo Oktoba 04, 2023 katika hafla iliyofanyika katika Ofisi ndogo za  Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu nchini (HESLB) Dar es Salaam.

Prof. Mkenda ameeleza kuwa uamuzi huo umefikiwa kufuatia marekebisho ya sheria ya HESLB, mwaka 2017.

Ameyataja maeneo ya kipaumbele kuwa yamegawanyika katika maeneo saba i.) Afya na Sayansi Shirikishi. ii.) Elimu (Stashahada ya ualimu wa masomo ya fizikia, hisabati na aamali). iii.) Usafiri na Usafirishaji (Transport & Logistics). iv.) Uhandisi wa Nishati (Energy Engineering). v.) Madini na Sayansi ya Ardhi (Mining and Earth Science), na vi.) Kilimo na Mifugo (Agriculture & Livestock).

Aidha, kiongozi huyo amewaasa wazazi na walezi kushirikiana na watoto wao katika kusoma kwa makini muongozo huo, kwani itawepesisha kujua ni eneo gani limepewa sifa zaidi na viambatanisho muhimu ili kunufaika na mkopo huo.

“Muongozo utaanza kupatikana kwa lugha ya Kiswahili kuanzia leo, kupitia tovuti za Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (www.moe.go.tz), HESB (www.heslb.go.tz) tovuti ya Baraza la Taifa la Elimu ya Mafunzo ya Ufundi Stadi (www.nacte.go.tz),” amesema Prof. Mkenda

Aidha, Waziri huyo amesema wanatoa siku nne kwa wanafunzi wakisimamiwa na wazazi au walezi kusoma muongozo huo kwa makini kisha Oktoba 7, 2023 dirisha la kupokea maombi kwa njia ya mtandao litakuwa wazi na litadumu kwa siku 15, ambapo ni sawa na Oktoba 22, 2023.

“Maombi yote ya mikopo yatafanyika kwa njia ya mtandao kupitia www.olas.heslb.go.tz waombaji mkopo hawatapaswa kutumia nakala ngumu ‘hardcopy’ au kufika ofisi za bodi, badala yake watatuma nakala laini tu ‘soft copy’. ” Amesema Prof. Mkenda.

Aidha, amesema mwanafunzi ili kuomba mkopo atafungua akaunti ya SIPA ambayo pia itamuwezesha kufuatilia mwenendo wa mkopo.

“Baada ya kumaliza masomo mwanafunzi-mnufaika atapaswa kurejesha mkopo kwa kiwango cha asilimia 15 kutoka kwenye mshahara wa mwezi.” Amesema kiongozi huyo.

Itakumbukwa, huu ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan kutaka wanafunzi wa vyuo vya kati kunufaika na mikopo ya serikali ikiwa ni utekelezaji wa maazimio ya Afrika kuhusu rasilimali watu.

Hii ni mara ya kwanza kwa HESLB kutoa mikopo kwa wanafunzi wa ngazi ya Stashahada, ingawa kupitia mfuko wa kuwainua kimasomo wanafunzi wanaofanya vizuri katika masomo ya kipaumbele (Samia Scholarship), Serikali imepanua mfuko huo kufikia Sh bilioni 6.7 ikiwa ni mwaka wa pili wa utekelezaji wake.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button