Wanafunzi wa kike washauriwa kuziishi ndoto zao

PWANI: WANAFUNZI wa kike wameshauriwa kusoma kwa bidii na kuepuka tamaa zinazoweza kuwasababishia kupata ujauzito na hatimaye kukatiza masomo.
Mwanafunzi Ruth Waluye ambaye anasoma kupitia Mradi wa Kuimarisha Ubora wa Elimu ya Sekondari na Program ya Elimu ya Sekondari kwa Njia Mbadala (Sequip- AEP), ameshauri hayo katika Maadhimisho ya Juma la Elimu la Watu Wazima Kitaifa, yanayofanyika Kibaha Pwani.
“Ninachowashauri wale walioko shule wawe makini na masomo, na wale waliopatwa na tatizo la ujauzito wasiogope na kujificha nyumbani bali warudi kuendelea na masomo,” amesema.
Amesema alikatiza masomo akiwa kidato cha tatu baada ya kupata ujauzito, hivyo mwaka jana aliposikia Rais Samia Suluhu Hassan amewataka wanafunzi waliopata ujauzito kurudi shuleni, alirudi kwa mfumo huo wa Sequip.
Amesema awali alisoma shule ya Sekondari ya Wasichana Kibaha hivi sasa anasoma katika Shule ya Sekondari ya Tumbi chini ya mradi huo wa Sequip, anasoma mfumo wa miaka miwili na mwaka huu anamaliza masomo yake katika mfumo wa elimu ya sekondari kwa njia mbadala.
“Baada ya kukatiza masomo nilijisikia vibaya, jamii iliniangalia na kuzungumza maneno mengi. Nia yangu ilikuwa ni kusoma, sikulazimishwa nilirudi mwenyewe shule,” amesema.
Naye Selina Assenga amesema aliacha masomo baada ya baba yake kufariki, huku mama yake akiwa anasumbuliwa na maradhi mbalimbali hivyo aliamua kurudi shuleni.
Kwa upande wake Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima Profesa Michael Ng’umbi amesema maadhimisho hayo ni mojawapo ya jitihada za kukumbusha jamii kuhusu umuhimu wa elimu ya watu wazima.
“Na imefanywa hivyo kwa sababu ni wajibu wetu kuhamasisha jamii kuona kwamba elimu ya watu wazima bado ni nyenzo muhimu katika kujenga utu na kuhakikisha kwamba haki ya msingi ya binadamu ya kujua kusoma, kuandika na kuendelea kujifunza muda wote inazingatiwa,” amesema.
Amesema katika juma hilo wameonesha program ya sekondari kwa vijana walio nje ya shule kwa maana elimu ya sekondari nje ya mfumo rasmi inayowawezesha wasichana kurudi kwenye mfumo wa shule baada ya kuacha.
Kwa upande wake Naibu Mkuu wa Taasisi upande wa Taaluma, Utafiti na Ushauri, Dk Philipo Sanga amesema umuhimu wa maadhimisho hayo inaifanya jamii kukumbusha elimu ya watu wazima katika maendeleo ya jamii.



