‘Waelimisheni wanawake wajiunge majukwaa ya uwezeshaji’
SERIKALI imezindua mwongozo wa kitaifa wa uanzishaji na uendeshaji majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi, wenye lengo la kuleta ufanisi wa utekelezaji wa majukwaa hayo, ikiwa ni pamoja na kuyafanya yajulikane katika ngazi zote nchini.
Akizungumza katika uzinduzi wa mwongozo huo kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dk. Dorothy Gwajima, ameitaka jamii kuelimisha wanawake juu ya umuhimu wa kujiunga na majukwaa hayo kuanzia ngazi ya kijiji/mtaa, kata, wilaya hadi taifa.
Waziri Gwajima amesema majukwaa hayo yatatoa fursa kwa wanawake kujadili mambo yao hususani masuala ya ujasiriamali na biashara kwa ujumla
“Halmashauri za Wilaya/Manispaa na Majiji ziendelee kutenga fedha za ndani ili kuwawezesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kukopa na hatimaye kuweza kujiendeleza kiuchumi,” alisema Waziri Gwajima.
Pia ametoa rai kwa wanufaika wa mikopo ya asilimia 10 na mikopo ya Maendeleo ya Wanawake (WDF), inayotolewa na Wizara wahakikishe wanarejesha mikopo hiyo kwa wakati, ili iwezeshe kuwanufaisha wengine kupata mikopo mapema.
Dk. Gwajima ametoa wito kwa wanawake na wanaume, kuzidi kuungana kupinga ukatili wa kijinsia na kwa watoto kwa kusimamia kurithisha misingi ya maadili mema kwa vizazi vijavyo.



