Mashirika Afrika yataka lugha yenye nguvu udhibiti nishati chafu COP28

WAKATI Mkutano wa Mabadiliko ya tabianchi (COP28) unatarajiwa kufungwa kesho ,Dubai Falme za Kiarabu Mashirika ya Kiraia ya Afrika (CSOs) na wawakilishi kutoka jamii zilizoathirika wametoa wito kuwepo kwa kauli yenye nguvu juu ya nishati chafu na kuongezeka mara tatu kwa nishati mbadala barani Afrika kwa kuongeza fedha.
Wakizungumza na waandishi wa habari pembezoni mwa mkutano huo mashirika hayo yamehimiza mazungumzo ya kusukuma matokeo ambayo yataleta mabadiliko ya haraka ya haki na yanayofadhiliwa kikamilifu kutoka kwa wazalishaji wa nishati chafu.

Hatua hiyo imekuja baada ya athari ya mabadiliko ya tabianchi ikiwa ni pamoja na mafuriko yanayoshuhudiwa hivi sasa Afrika Mashariki ambayo yamegharimu maisha ya zaidi ya watu 350 na kusababisha watu milioni moja kuyahama makazi yao nchini Kenya na Tanzania.
Mshauri Mkuu wa Marekebisho na Ustahimilivu wa Shirika la Umoja wa Mataifa, Christina Rhumbaitis amesema lengo la Kimataifa la kukabiliana na hali ya uzalishaji nishati chafu ni matokeo muhimu zaidi yanayotarajiwa kuonekana katika COP28.
“Tunahitaji mfumo huu, wenye malengo ya wazi na ufadhili nyuma yake kuwa elekezi kwa ajili ya kukabiliana na hali hiyo ambapo mfumo lazima utume ujumbe wazi kwa wanasiasa na watoa maamuzi katika ngazi zote kwamba hatua za haraka zinahitajika ili kupata hali ya hewa nzuri.
Kwa upande wake,Mkuu wa masuala ya Mpito ya Nishati ya Utafiti kutoka Taasisi ya Power Shift Afrika, Amos Wemanya amesema COP28 si mahali pa kulinda maslahi ya mtu binafsi au ya nchi inapaswa kuwa mahali pa kuunda ushirikiano ambao unaruhusu nchi zote kuondokana na nishati chafu.

“Ni wakati wa kila mtu katika COP hii kutaka mfumo wa nishati ambao unawajibika kwa athari ya hali ya hewa ambayo ulimwengu unapitia hivi sasa na tunajua chanzo cha mzozo wa hali ya hewa lazima tushughulikie uzalishaji kutoka kwa chanzo,”ameeleza.
Florence Gichoya kutoka Muungano wa ACCESS amebainisha kuwa ili kufikia mabadiliko ya haki katika nishati inahitaji kuchukua mbinu inayozingatia mahitaj kwa bara la Afrika.
“Jamii tofauti zina mahitaji tofauti ya nishati hivyo njia za mpito tunazokuza lazima zikidhi mahitaji haya na ni lazima tuwe na mtumiaji wa mwisho akilini huku tukitengeneza njia zozote za nishati ili ziwe sawa kwa wote kwani kila maamuzi yanayofanyika hapa COP28 yanamatokeo sio tu kwetu hata kwa kizazi kijacho.

Katika Azimio la Nairobi la Mkutano wa Kilele cha mabadiliko ya tabianchi barani Afrika, viongozi wa Afrika walibainisha kuwa kufikia lengo la nishati mbadala ifikapo mwaka 2030 kunahitaji wastani wa dola bilioni 600, ambayo ina maana ya ongezeko mara kumi ya fedha zinazoingia katika sekta ya nishati mbadala ya Afrika katika miaka saba ijayo.
Habari hii imewezeshwa na MESHA na Ofisi ya Afrika ya IDRC Mashariki na Kusini.



