Wamiliki leseni za madini wapewa maagizo
LINDI: WAMILIKI leseni za madini nchini wametakiwa kuziendeleza la sivyo watafutiwa leseni hizo kwa mujibu wa sheria.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde Ruangwa mkoani Lindi katika ziara yake kwenye mgodi wa Kinywe .
Mavunde amesema kuwa zipo leseni nyingi ambazo hazifanyiwi kazi na hivyo kuzorotesha ukuaji wa kasi wa sekta ya madini.

“Nitumie fursa hii kuwatangazia wale wamiliki wa leseni wasiondeleza maeneo yao kuzingatia matakwa ya sheria juu ya umiliki wao wa leseni husika vinginevyo leseni hizo zitafutwa kwa mujibu wa sheria,” amesema Mavunde na kuongeza
” Tutatoa nafasi kwa watu wanaoweza kuendeleza,kwa kuwa kwa hivi sasa wapo watu wengi wanashikilia maeneo makubwa ya madini pasipo kuyafanyia kazi na kuwanyima fursa watu wengi zaidi kushiriki katika uchumi huu, ” amesisitiza.
Aidha, akizungumzia mradi wa mgodi wa Kinywe Mavunde amesema mradi huo utakuwa kati ya miradi michache mipya ya uchimbaji wa madini mkakati ya kinywe nchini Tanzania ambao utakuwa umeanza hivi karibuni.

“Dhamira ya serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ni kuona shughuli za uchimbaji wa madini zinaongezeka ili kuchochea ukuaji wa sekta ya madini na kuleta matokeo chanya kwenye uchumi wa nchi na kuongeza nafasi za ajira, “amesema.
Awali, akitoa taarifa ya Mradi wa mgodi huo,Meneja Msimamizi, Mhandisi Chediel Mshana amesema ujenzi wa mgodi huo umefikia asilimia 90 na kwamba ifikapo mwezi Machi,2024 mgodi utakuwa umeanza uzalishaji rasmi wa madini ya kinywe.

Naye Mkuu wa Wilaya wa Ruangwa, Hassan Ngoma amesema kukamilika kwa mradi huo kutachochea ukuaji wa sekta ya madini na maendeleo katika wilaya hiyo kuahidi kufanyia kazi changamoto ya barabara inayoenda mgodini hapo ili kurahisisha shughuli za uchimbaji madini.



