Ujenzi miundombinu kuvutia wawekezaji
MKAKATI wa serikali ni kuhakikisha inajenga miundombinu wezeshi ili kuvutia wawekezaji katika maeneo mbalimbali nchini, bunge limeelezwa.
Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe alisema hayo jana wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kigoma Kusini, Nashon Bidyanguze (CCM).
Mbunge huyo alisema Uvinza inapatikana malighafi ya saruji na kutaka kufahamu ni lini serikali itakwenda kuwekeza kiwanda ili kutoa fursa za ajira na kukamata soko la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Burundi.
Akijibu swali hilo, Kigahe alisema kwa sasa mkakati wa serikali ni kuhakikisha inajenga miundombinu wezeshi kuvutia wawekezaji na kuwa hata Uvinza miundo ikishakuwa vizuri viwanda vitajengwa kwa wingi.
Katika swali lake la msingi, Bidyanguze alitaka kufahamu serikali itapeleka lini mwekezaji wa kiwanda cha saruji katika Wilaya ya Uvinza.
Akijibu swali hilo, Kigahe alisema serikali inatekeleza mikakati mbalimbali ili kuhamasisha na kuvutia wawekezaji ikiwemo kwenye sekta ndogo ya saruji nchini.
Alisema Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kwa kushirikiana na uongozi wa Mkoa wa Kigoma kimeweza kuvutia mwekezaji (Itracom Fertilizer) kujenga kiwanda cha saruji na kumpa ekari 47 katika Eneo la Uwekezaji la Kigoma (KiSEZ).
Kigahe alisema Wilaya ya Uvinza pia itanufaika na mwekezaji huyo na kuwa serikali inaendelea kuvutia wawekezaji zaidi ili kuwekeza katika Mkoa wa Kigoma ikiwemo Wilaya ya Uvinza.



