Wafanyabiashara Katavi waomba elimu TRA

KATAVI: Wafanyabiashara wa Wilaya ya Mlele Mkoa wa Katavi wameomba kupatiwa elimu endelevu kutoka kwa Mamkala ya Mapato Tanzania (TRA) ili kuweza kupata uelewa mpana kuhusu mamlaka hiyo.
Ombi hilo wamelitoa katika kikao cha wafanyabiashara wa Kata ya Majimoto na maofisa kutoka makao makuu ya TRA, jijini Dar es Salaam kilichofanyika katika Ukumbi wa Gwambina ambapo maofisa hao walipata nafasi ya kutoa elimu ya ulipaji kodi na kusikiliza changamoto mbalimbali za kikodi ili kuweza kuzifanyia kazi.
Aidha, wafanyabiashara wamesema awali walikuwa wakihisi kukandamizwa na TRA pindi wanapofanyiwa makadirio ambapo baada ya elimu hiyo wamepata ufahamu hususani kwenye suala la namba ya utambulisho wa mlipakodi yaani TIN.
“Nimejifunza mambo mengi zamani nilikuwa najua TIN zinauzwa baada ya elimu hii nimegundua kuwa TIN haiuzwi,lakini pia tunaomba kutatuliwa changamoto zetu ambazo tulishawahi kuziwasilisha TRA mkoa” amesema Johari Mohamed ambaye ni mfanyabiashara Kata ya Majimoto
Akizungumza katika kikao hicho Mbunge wa Jimbo la Kavuu, Geofrey Pinda ameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wilayani Mlele kujenga uhusiano mzuri na wafanyabiashara waliopo Kata ya Majimoto ili kuwasaidia na kuwawezesha kuendelea katika biashara zao.
Aidha Pinda ameahidi kushiriki katika kutatua changamoto ya ofisi ya TRA wilayani hapo kwa kutoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa ofisi hiyo huku akiahidi pia kutoa ushirikiano kwa TRA endapo utahitajika.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Majid Mwanga amewataka wafanyabiashara kulipa kodi kwa hiyari na kwa wakati sambamba na kutoa risiti halali za kielektroniki kwa mauzo wanayofanya ili kuwezesha Serikali kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.
Timu ya maofisa kutoka makao makuu ya TRA jijini Dar es Salaam imefunga kambi katika Mkoa wa Katavi kwa muda wa wiki mbili kwa lengo la kuwafikia wafanyabishara mkoani hapo hususani Wilaya ya Mlele kwa lengo kuwapa elimu ya ulipaji kodi sambamba na kusikiliza changamoto ili kuweza kuzifanyia kazi.



