Wachakataji dagaa waomba uwekezaji nishati umeme jua

ANASEMA ufanisi wa teknolojia ya kitalu nyumba ukiweka tani mbili za dagaa kwenye mtambo, baada ya kukauka hubakia tani moja kwa sababu huondoa unyevu wote na hutunza rangi ya bidhaa husika. Shirika la Chakula na Kilimo duniani (FAO) limetilia mkazo suala la kuongeza matumizi ya teknolojia kwa ajili ya uanika[1]ji dagaa, kwa lengo la kuboresha usalama na ubora wa dagaa pamoja na kukabiliana na uharibifu wa mazingira ifikapo mwaka 2025.

Pia, limetaka ifikapo mwaka 2030 kupunguza upotevu wa mazao ya uvuvi kwa asilimia 60. Takwimu za Wizara ya Mifugo na Uvuvi, zinaonesha kuwa asilimia 70 ya dagaa hupotea kwa kipindi cha mvua na asilimia 40 kwa kipindi kisichokuwa na mvua kutokana na uanikaji wa kwenye vichanja na kwenye mawe pamoja na uhi[1]fadhi usioridhisha huku zaidi ya Sh bilioni 79 zikipotea kila mwaka.

Kutokana na hali hiyo, Mwaka 2022/2023 Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) ilifanya utafiti kubaini upotevu wa ubora kwenye mnyororo mzima wa thamani kutoka wanapovuliwa hadi kuhifadhiwa.

Utafiti huo umeonesha kuwa toka dagaa wanapovuliwa hadi kufika mwaloni kuna upotevu wa asilimia 21 wakati mchuuzi anapoteza asilimia 39 ya dagaa.

Wavuvi na wachakataji wa dagaa katika mwalo wa Kayenze ndogo, wanasema upotevu wa dagaa huchangiwa na kukosekana kwa vifaa bora vya uhifadhi na kukausha hususani hali ya hewa inapo[1]badilika.

Mmoja wa wavuvi hao, Mabula Nyanda aliomba wadau ili kukabiliana na upotevu huo na kuwasaidia waendeleze biashara hiyo ambayo inawaingizia kipato na kuchangia kwenye Uchumi wa nchi. Faustine Frank anasema mavuno mengi ya dagaa hupatikana wakati wa mvua na ili waweze kukabiliana na upotevu, wana[1]hitaji vifaa vya kisasa kwa ajili ya kukausha na kuhifadhi kwa muda mrefu.

“Natumia taa ya umeme jua wakati wa uvuvi usiku, napata dagaa wengi ambao nikiwauza wananisaidia kukuza kipato changu, ninasomesha na kupata mahitaji mengine kutokana na dagaa,” anaeleza Frank.

Naye, Yohana Masanja anasema anatumia barafu kwa ajili ya kuhifadhi dagaa wake baada ya kuvua na kwamba bila ku[1]fanya hivyo, hadi wanapotoka mawindoni (kuvua) wanaweza kuharibika.

Mwenyekiti wa Kikundi cha wachakataji wa dagaa Kayenze, Mektrida Jacob anasema kikundi hicho kina zaidi ya wanawake 50 ambao wanafanya kazi ya kukausha dagaa kwenye mawe, vichanja na mitambo ya umeme jua.

Anasema kuwa wanaamka saa 8 usiku kwenda kushiriki mnada wa dagaa na kisha yeyote anayefanikiwa kupata dagaa kwenye mnada huo, huanika kwa namna anavyotaka. Jacob anasema wanapata wateja kutoka maeneo mbalimbali na kwamba wanauza kwa bei tofauti kulingana na majira na ubora wa dagaa hao.

“Ndoo ya dagaa wenye mchanga bei yao ni ya Sh 6,000 kwa sababu hawana ubora mzuri na wale wasio na mchanga ambao tunaanika kwenye vichanja wanaweza kufika Sh 32,000.

Maziwa ya Nyasa na Tanganyika yakifungwa, tunapata wateja wengi,” anasema. Hatua ya kufungia maziwa ni mkakati wa serikali wa upumzishwaji wa shughuli za uvuvi kwa lengo la kuruhusu samaki na mazao ya uvuvi kuzaliana, kuimarisha bayoanuai na kuongeza uzalishaji wa samaki ili kuwa na uvuvi endelevu na wenye tija.

Anaongeza kuwa kipindi cha mvua dagaa wanaokaushwa kwa njia za asili ikiwemo mawe na vichanja, huwa chakula cha kuku ambacho huuzwa kati ya Sh 6,000 hadi 7,000 kwa ndoo.

Mkakati kupunguza upotevu Kutokana na upotevu huo, serikali ilikuja na Mkakati wa Kupunguza Upotevu wa Mazao ya Dagaa wa mwaka 2023 hadi 2030 ambao umelenga kupunguza upotevu wa dagaa kwa asilimia 60 na kumuwezesha mchuuzi kupunguza hasara kutoka asilimia 39 hadi 21.

Mkakati huo unapendekeza matumizi ya nishati safi ya umeme jua kwa ajili ya kusaidia ukaushaji wa dagaa, utunzaji kwenye baridi ili dagaa hao waweze kuwa salama kwa matumizi na kupunguza upotevu.

Aliyekuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega alisema kuwa yapo maeneo mbalimbali yanayozunguka Ziwa Victoria ambayo tayari yameanza matumizi ya teknolojia ya vitalu nyumba kukaushia dagaa “Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Kilimo (IFAD) chini ya Mpango wa Maendeleo ya Kilimo na Uvuvi (AFDP -2027) wameomba wakandarasi wenye uwezo wa kutengeneza mitambo ya nishati ya umeme jua, ili kukausha dagaa,” alifafanua Ulega.

Mkurugenzi wa Nishati Jadidifu kutoka Wakala wa Umeme Vijijini (REA), Advera Mwijage anasema nishati jadidifu ina mchango mkubwa kwa kuwa ni rafiki wa mazingira hivyo huongeza ubora wa dagaa na kuwezesha kupenya kwenye masoko ya kimataifa.

“Serikali inatoa ruzuku kwa kampuni ambazo zinataka kuweka teknolojia hiyo kwenye mialo mbalimbali iliyopo Ziwa Victoria na maeneo mengine nchini,” anasema Mwijage.

Faida ulaji dagaa Zipo faida nyingi za kutumia dagaa kwani wana kiwango kikubwa cha protini ambacho ni muhimu kwa ukuaji wa misuli, ukarabati wa tishu, na kuboresha kinga ya mwili.

Protini pia husaidia katika uzalishaji wa homoni na vimeng’enya mwilini. Kwa mujibu wa Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Lishe kutoka Wizara ya Afya, Neema Joshua anasema dagaa wana kiasi kikubwa cha kalsiamu muhimu kwa kuimarisha mifupa na meno na husaidia katika kuepuka matatizo ya mifupa kama vile ugonjwa wa ‘Osteoporosis’.

Joshua anasema dagaa ni muhimu kwa utengenezaji wa seli nyekundu za damu, afya ya mfumo wa neva, na husaidia kuzuia upungufu wa damu (anemia) kutokana na kuwa na Vitamin B12 na madini chuma kwa wingi. Faida nyingine ni kuwa dagaa wana mafuta ya Omega-3 muhimu yanayosaidia afya ya moyo kwa kupunguza viwango vya mafuta mabaya (lehemu) mwilini na kusaidia kupunguza hatari ya magonjwa ya moyo. Pia, husaidia katika ukuaji wa ubongo na kuboresha afya ya akili.

Anasema kuwa Vitamini A kutoka kwa dagaa ni muhimu kwa afya ya macho, ngozi, na mfumo wa kinga, husaidia mlaji kuepuka matatizo ya kuona usiku na ku[1]boresha afya ya ngozi. “Inashauriwa kula dagaa na vichwa vyake kwani Vitamin A nyingi na madini ya Zinki yanapatikana hapo,” anasema Joshua.

Habari Zifananazo

Back to top button