MPOGOLO: Msichonge mihuri, subirini miongozo

DAR ES SALAAM: MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amewataka wenyeviti wote wa serikali za Mitaa wilayani humo kusubiri muongozo wa upatikanaji wa mihuri kutoka katika Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam, hivyo aliwataka waache kuchonga mihuri hadi miongozi itakapotolewa.
Mpogolo ametoa agizo hilo Desemba 18, 2024 wakati akifunga mafunzo kwa wenyeviti wa serikali za mitaa 159 kutoka katika Kata 36 zililizopo ndani ya Wilaya ya Ilala waliochaguliwa hivi karibuni katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
Mpogolo amesema Halmashauri ya Jiji ndiyo itakayotoa mihuri itakayotumika, hivyo ni kosa kwa Mwenyekiti kuchonga mhuri bila ridhaa ya serikali na kuanza kuitumia.

Aidha, amesema mhuri ni nyaraka ya serikali na ndiyo yenye dhamana ya kuiandaa na kukabidhi kwa watumishi wake kwa ajili ya kuwahudumia wananchi.
Mpogolo amesema mafunzo hayo yamelenga yamelenga kujua wajibu wa viongozi, mahusiano na muundo wa serikali za mitaa katika usimamizi wa miradi ya maendeleo, ulinzi na usalama, na kukusanya mapato.
Akizungumzia juu ya usafi wa mazingira Mpogolo ameeleza wenyeviti wakasimamie usafi kwa kushirikiana na wakandarasi na wananchi wawe tayari kushiriki zoezi ilo.
Pia katika mafunzo hayo ameeleza mpango mkakati wa kuhakikisha wafanyabiashara wa soko la kariakoo wasio katika maeneo rasmi kurejeshwa katika maeneo waliopangiwa awali.

Mpogolo amesema zoezi hilo linakwenda sambamba na kuwaondoa wafanyabiashara wa pembezoni mwa barabara na kupiga marufuku kuingia na vyombo vya moto katikati ya soko la kariakoo kuanzia siku ya ijumaa.
Aidha mafunzo hayo kwa Wenyeviti wa serikali za mitaa toka halmashauri ya jiji la Ilala yameendeshwa na wakufunzi toka chuo cha Serikali za mitaa Homboro ili kuwajengea uwezo viongozi hao katika kuwatumikia wananchi kwa kipindi cha miaka mitano.



