RC Mtwara ataka ufuatiliaji wa miradi

MKUU wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala amezitaka idara zinazohusika na usimamizi wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani humo kuwa na ufatiliaji wa karibu kwenye miradi hiyo ili mwisho wa siku wafurahie kazi kubwa iliyofanyika.
Akizungumza leo mkoani Mtwara alipotembelea miradi hiyo ya maendeleo inayotekelezwa kwenye manispaa hiyo, Mkuu huyo wa Mkoa amesema kuwe na usimamizi wa karibu lakini kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo iongezwe ili wananchi waendelee kufurahia huduma hizo.

Aidha katika ziara hiyo miradi iliyotembelewa ni minne ikiwemo ujenzi wa jengo la ofisi ya kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa mtwara (RPC) unaokadiriwa kugharimu zaidi ya Sh bilioni 1.6, ujenzi wa madarasa mawili na matundu sita ya vyoo katika shule ya msingi magomeni uliyogharimu zaidi ya Sh milioni 58.
Miradi mingine ni wa uboreshaji wa mfumo wa usambazaji maji mjini Mtwara unaosimamiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mtwara (MTUWASA) utaogharimu zaidi ya Sh bilioni 29 hadi kukamilika kwake.

Hata hivyo ujenzi wa hospitali ya halmashauri hiyo ya manispaa ya mtwara mikindani uliyopo mjimwema kwenye manispaa hiyo itaogharimu zaidi ya Sh bilioni 3.
‘’Idara tumizi tuwe karibu kuwashauri mafundi na wahandisi kuwa hapa panatikiwa kitu hiki isije kuwekwa kitu ambacho siyo sahihi halafu baadaye inakuja kuanza gharama mara mbili za kuanza kubomoa tena’’amesisitiza Sawala .

Hata hivyo Sawala ameridhishwa na hali ya utekelezaji wa miradi yote minne aliyoitembelea huku akisisitiza suala la kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ili iweze kuendana na wakati na kwa ubora unaotakiwa.



