Mradi ‘Mama Jasiri’ kuimarisha wanawake wazalendo Tz

TANZANIA na Uturuki zimeimarisha ushirikiano wao kwa kuzindua rasmi mradi wa ‘Mama Jasiri’ unaolenga kuwawezesha wanawake kiuchumi na kijamii kwa njia endelevu.
Balozi wa Uturuki nchini, Dk Mehmet Güllüoğlu, amesema kuwa mradi huo si wa kawaida bali ni nguzo muhimu kwa wanawake wadogo wanaokabiliwa na changamoto za maisha.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi iliyofanyika Wilaya ya Kinondoni, Dk Güllüoğlu amesisitiza umuhimu wa kudumisha mradi huo ili kuhakikisha unaleta manufaa ya kudumu kwa jamii. “Mradi huu unawakilisha tumaini jipya kwa wanawake wa Kitanzania. Tunapowekeza katika maisha yao, tunawekeza kwenye mustakabali wa taifa letu. Uendelevu ni msingi wa mafanikio yake,” alisema.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali, akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, ambaye ameeleza kuwa mradi huo ni mkombozi kwa wanawake wengi waliokosa elimu na ajira.
Alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi za kufungua milango ya ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Uturuki, huku akiahidi kwamba wilaya hiyo itasimamia utekelezaji wa mradi kwa ufanisi.
Makamu wa Rais wa TIKA, nurdun Rahman amebainisha kuwa wanawake wana nguvu ya kipekee ya kubadilisha dunia, na mradi wa Jasiri unalenga kufanikisha hilo. “Tumejumuisha wanawake kutoka mazingira mbalimbali na kuwapa fursa za kipekee kupitia mradi huu. Tunaamini jitihada zao zitakuwa chachu ya mabadiliko makubwa,” alisema Başar.

Kwa upande wake, Zeliha Sağlam, Mkuu wa Africa Culture House kutoka Uturuki, ameelezea kuwa taasisi hiyo inashirikiana na serikali za Afrika, ikiwemo Tanzania, kukuza vipaji vya wanawake kupitia miradi kama Jasiri. “Tunaamini katika uwezo wa wanawake wa Afrika na tunaahidi kuwa nao bega kwa bega katika kukabiliana na changamoto mbalimbali wanazokutana nazo,” amesema Sağlam.
Mradi wa Jasiri unaashiria dhamira ya dhati ya nchi hizi mbili katika kuhakikisha kuwa wanawake wanakuwa na nafasi sawa za kushiriki katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii, huku ukitoa msingi madhubuti wa ustawi wa jamii kwa vizazi vijavyo.



