Daladala 37 zasaidia mwendokasi Mbezi

DAR ES SALAAM: DALADALA 37 zimepatiwa leseni za muda kwa ajili ya kutoa huduma za usafiri barabara ya Morogoro sambamba na Mabasi Yaendayo Haraka, maarufu mwendokasi ili kukabiliana na changamoto ya usafiri.

Ikumbukwe tangu mradi wa mabasi ya mwendokasi uanze rasmi mwaka 2016, daladala ambazo zilikuwa zikifanya safari zake kutoka Mbezi Luis kwenda katikati ya Dar es Salaam zilisitishwa.

Sababu ya kusitisha kwa usafiri wa daladala katika njia hiyo ni kuruhusu usafiri huo kutoa huduma na kwamba barabara zake zilivyosanifiwa hazikuwa na vituo vya daladala.

Akizungumza na HabariLEO jana, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA), Salum Pazzy alisema idadi ya leseni za muda walizotoa zimeongezeka kutoka 15 Oktoba mwaka jana hadi 37, mwaka huu.

Kwa mujibu wa leseni hizo, daladala zinatakiwa ziwe na uwezo wa kubeba abiria kuanzia 25 na zitaongeza leseni kulingana na mahitaji ya huduma za usafiri.

Pazzy alisema daladala zitakuwa zikifanya safari zake Mbezi Luis kwenda Makumbusho kupitia Barabara ya Morogoro, Magomeni na Mwananyamala.

Pia, kutoka Mbezi Luis kwenda Mwenge kupitia barabara ya Sam Nujoma, kutoka Mbezi Luis kwenda Mnazi Mmoja kupitia Barabara ya Morogoro, Nelson Mandela na Uhuru pamoja na Mbezi Luis kwenda Mnazi kupitia Kwa Mkua.

“Tunaamini uwekezaji uliofanywa na serikali katika ujenzi wa miundombinu ya barabara za mwendokasi ikikamilika na akipatikana mwekezaji wa kutoa huduma za usafiri au UDART ikiongeza huduma, usafiri Dar es Salaam utakuwa mzuri,” alisema Pazzy.

Maamuzi ya kuanza kutolewa kwa leseni hizo yalitokana na tamko la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ambaye alitembelea Kituo cha mabasi ya mwendokasi cha Kimara ambacho kilikuwa na changamoto ya msongamano wa abiria huku magari hayo yakiwa machache.

Katika ziara ya Chalamila, baadhi ya maoni ya wananchi aliyoyakusanya yalihusu kuwapo kwa mshindani katika barabara ambayo magari ya mwendokasi pekee yanapita.

Hata hivyo, kutokana na changamoto za usafiri huo wa mwendokasi unaosababisha abiria kukaa vituoni muda mrefu, abiria wamekuwa wakitumia usafiri wa kukodi wa bajaji au bodaboda ambao nauli yake ni kati ya Sh 2,000 hadi Sh 3,000.

Habari Zifananazo

Back to top button