Dachi ataja malengo ya TSN 2025

DODOMA; MKURUGENZI Mtendaji wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), Asha Dachi amesema mwelekeo wa kampuni kwa mwaka 2025 ni kukuza biashara ya magazeti na kuendelea kuwa daraja kati ya wananchi na serikali yao.
Dachi ameyasema hayo jana wakati wa kutoa salamu za heri kwa kuuaga mwaka 2024 na kuukaribisha Mwaka Mpya wa 2025.
Alisema kampuni hiyo imeweka mkakati wa kukuza biashara ya magazeti, kuwa daraja kati ya serikali na wananchi bila kusahau ushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa 2025.
“Watanzania watarajie makubwa kutoka TSN kwa sababu mwaka 2025 tunaenda kidigitali zaidi ili tuweze kuwafikia Watanzania wengi. Tunaamini katika mfumo wa kidigitali basi huko ndio waliko watanzania wengi hasa vijana,” alisema Dachi.
Aliongeza: “Tunaenda kuimarisha zaidi uuzaji wa gazeti kwa njia ya mtandao na kuimarisha kurasa za mitandao ya kijamii za X, Instagram, Facebook na YouTube kwa kuwaletea maudhui yaliyo bora zaidi”.

Aidha, Dachi alisema mwaka 2024 ulikuwa ni mwaka wa mafanikio hasa katika kutekeleza dhima yake ya kuwa daraja kati ya wananchi na serikali yao.
“Tumetekeleza mambo kadhaa, ikiwamo kuwaelimisha Watanzania kuhusu utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025 na maandalizi ya Dira ya mwaka 2050. TSN imekuwa mstari wa mbele kuhakikishia Watanzania wanashiriki kikamilifu na kukusanya maoni yao na kupeleka kwa mamlaka husika inayokusanya maoni kuhusu dira mpya,” alifafanua Dachi.
Alisema kupitia magazeti na kurasa za mitandao ya kijamii ya kampuni wameelezea wananchi juu ya miradi ya kimkakati inayotekelezeka na serikali na bila kusahau utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya 2020-2025



