Msigwa ahimiza ubunifu TSN

DAR ES SALAAM; Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa amehimiza watumishi wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) kuongeza nguvu kwenye ubunifu, ili kuzidi kuipaisha kampuni hiyo.
Msigwa ambaye pia ni msemaji mkuu wa serikali, amesema hayo leo Januari 3, 2024 alipofika makao makuu ya kampuni hiyo eneo la Tazara, Dar es Salaam na kuzungumza na Menejimenti ya TSN, kisha kukagua mradi wa uchapaji kibiashara.

Amesema TSN ni kampuni kongwe na kuwapongeza kwa kuendelea kufanya kazi kwa weledi na kusisitiza kuwa kutokana na mabadiliko ya teknolojia ni wakati sasa wa kuongeza ubunifu katika kila eneo ili kufanya vizuri zaidi.
Amesema serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa TSN ili kurahisisha utendaji kazi wa taasisi hiyo na kuwataka watumishi kufanya kazi kulingana na malengo ya kuanzishwa kwake.

Amesema yapo matukio mbalimbali na kampeni tofauti za serikali ikiwemo ya matumizi ya nishati safi, hivyo ni jukumu la vyombo vilivyopo TSN kuwa mstari wa mbele kufanikisha kampeni hizo.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa TSN, Asha Dachi alimuelezea Katibu Mkuu huyo mikakati mbalimbali ambayo TSN imejiwekea katika kuendelea kuwa chombo cha kuaminika kwa umma kutokana na ubora wa habari zinazotolewa kwenye magazeti yake ya HabariLEO, DailyNews, SpotiLeo, mitandao ya kijamii ya magazeti hayo pamoja na chaneli ya DailyNews Digital.



