USAID Feed the Future yakomboa vijana wa Iringa

Iringa imeandika historia mpya kupitia mradi wa Feed the Future Tanzania Imarisha Sekta Binafsi, unaofadhiliwa kwa msaada wa watu wa Marekani kupitia USAID.
Mradi huu unalenga kuinua maisha ya vijana kupitia sekta za kilimo na ufugaji, huku ukiboresha mazingira ya biashara na kuleta matumaini mapya kwa wajasiriamali vijana.
Katika awamu hii, vijana 25 kutoka mkoa wa Iringa wamewezeshwa kwa ruzuku ya vifaa mbalimbali vya kisasa.
Miongoni mwa vifaa hivyo ni mashine za kutotolea vifaranga, majembe ya kukokotwa na ng’ombe, vifaa vya kufugia kuku na pampu za maji, na vingine vingi; vyote vikilenga kuongeza tija na ufanisi kwenye minyororo ya thamani ya kilimo na ufugaji.

Shirika la Agriedo Hub limekuwa mshirika muhimu wa mradi huu, likiwa limeongoza juhudi za kuwafikia vijana 700 katika mkoa mzima wa Iringa.
Mwakilishi wa Agriedo Hub, Felix Sigachumwa, alieleza kuwa katika awamu iliyopita, vijana wengine 75 walipata vifaa kama hivyo.
“Hawa vijana wamechangia asilimia 30 ya gharama ya vifaa na mradi umebeba asilimia 70. Hii inaonesha dhamira ya vijana wa Iringa ya kushiriki kikamilifu katika kuleta mabadiliko,” alisema Sigachumwa.
Mwakilishi wa USAID Feed the Future Tanzania, Isaya Mshindi, alisisitiza kuwa mradi huo unawaamini vijana kama chachu ya mabadiliko na ubunifu katika mifumo ya upatikanaji wa chakula.

“Tunapowekeza kwa vijana, tunawekeza kwenye maendeleo endelevu. Hawa ni viongozi wa kesho,” alisema.
Akigawa vifaa hivyo kwa vijana hao, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Kheri James, aliipongeza USAID kwa juhudi zake za kuboresha maisha ya vijana wa Iringa.
Alisema mradi huo umesaidia kuwawezesha vijana hao ukilenga kuimarisha biashara changa zinazohusiana na kilimo na ufugaji.
Hatua hiyo alisema inatarajiwa kuongeza ajira na kupunguza umasikini miongoni mwa vijana, sambamba na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika mkoa wa Iringa.
Alisisitiza kuwa vijana wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuchangamkia fursa na kuongeza ufanisi kwenye kilimo na ufugaji.
“Serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imepania kukuza sekta ya kilimo ili iwe na mchango mkubwa zaidi kwenye uchumi wa taifa kufikia mwaka 2030. Tunawahitaji vijana kama nyinyi kuwa mfano wa mabadiliko haya,” alisema James na kuongeza kwamba vijana waliopokea vifaa hivi wana matumaini makubwa.

“Vifaa nilivyopata vitanisaidia kuongeza uzalishaji na kipato changu,” alisema mmoja wa walengwa, Petro Valonge, kijana kutoka Iringa Mjini.
Naye Prisca Kaile alisema mradi huo si tu umewalenga wao kama vijana, bali utaleta mapinduzi makubwa katika mfumo wa kilimo na ufugaji, na kuwaonesha kuwa wao ni sehemu muhimu ya suluhisho la changamoto zinazolikumba taifa.



