Wafanyabiashara wavutiwa na biashara saa 24

DAR ES SALAAM; WAFANYABIASHARA kutoka baadhi ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) katika Soko la Machinga Complex lililopo wilayani Ilala mkoani Dar es Salaam wamevutiwa na utaratibu wa kufanya biashara kwa saa 24.

Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wadogo maarufu ‘Machinga’ katika Wilaya ya Ilala, Bakari Mkupa alisema mfumo wa kufanya biashara kwa saa 24 umevutia mataifa jirani hali iliyowafanya kuongeza bidii katika kuwapatia mahitaji yao.

Alisema kutokana na ongezeko la mataifa yanayokuja kuchukua mzigo nyakati za usiku ni dhahiri hata mzigo unaotoka usiku utakuwa umeongezeka na kuwa mkubwa zaidi ya ule unaotoka sokoni mchana.

“Kwa sasa kuna mataifa yaliyoongezeka ambayo ni Kenya, Uganda, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) mbali na yale ya awali ya Malawi, Zambia na Comoro, tunajitahidi kuwapatia mahitaji yao yote hapahapa usiku,” alisema Mkupa.

Alisema anaamini Soko la Kimataifa la Kariakoo litakapoanza biashara ya saa 24, mataifa mengi yataanza kufanya biashara usiku kwa sababu kuna utulivu mkubwa sokoni, lakini pia hata barabarani hakuna hekaheka nyingi.

Alisema sababu kubwa iliyowavuta wafanyabiashara wa nje kufanya biashara usiku ni kutokuwa na msongamano hali inayowarahisishia kufunga mizigo yao na kuondoka.

Hivi karibuni, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo alisema serikali imefanya majaribio ya biashara saa 24 katika soko hilo na kugundua changamoto kadhaa ambazo zinafanyiwa kazi kabla ya kuanza rasmi kwa biashara kwa saa 24 katika Soko la Kimataifa la Kariakoo.

Alibainisha kulingana na maandalizi yanavyokwenda, serikali inatarajia kuanza kwa mpango huo mwishoni mwa mwezi huu au mwanzoni mwa Februari 2025.

Aliongeza utekelezaji wa mpango huo utafanyika kwa umakini mkubwa kwa kushirikisha wadau wote wanaohusika kama vile wadau wa usafiri na usafirishaji pamoja na wamiliki wa majengo katika maeneo ya biashara.

Alisema baadhi ya changamoto zinazofanyiwa kazi ni kufunga taa na kamera katika maeneo yote yatakayotumika usiku kwa biashara na kuhimiza wenye nyumba wote wanaozunguka eneo hilo wafunge taa na kamera ili kuzidisha usalama katika maeneo yao.

Alifafanua serikali inaendelea kufanyia kazi miundombinu mbalimbali inayotakiwa kufanikisha mpango huo wa kufanya biashara kwa saa 24.

 

Habari Zifananazo

Back to top button