CONGO : Rais Tshisekedi asisitiza mapigano dhidi ya M23

CONGO : RAIS wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Felix Tshisekedi, amesema kuwa wanajeshi wa nchi hiyo wanapambana vikali kurejesha maeneo yaliyochukuliwa na waasi wa kundi la M23 linalosemekana kupata msaada kutoka Rwanda.
Kundi la M23 linadaiwa kutwaa maeneo makubwa ya mashariki mwa DRC, ikiwa ni pamoja na mji muhimu wa Goma.
Mashariki mwa Congo, ambapo kuna utajiri mkubwa wa madini, kumekuwa na mapigano makali yanayoendeshwa na makundi ya silaha, baadhi yao wakihusishwa na mauaji ya kimbari ya Rwanda mwaka 1994. SOMA: GOMA: Waasi wa M23 wateka uwanja wa ndege wa Goma

Akizungumza katika hotuba yake ya kwanza tangu kuanza kwa mgogoro huu, Tshisekedi alisema kuwa “jibu kali na lililoratibiwa dhidi ya magaidi hawa na wafuasi wao linaendelea.”
Rais Tshisekedi pia alikosoa jumuiya ya kimataifa kwa kushindwa kuchukua hatua. “Kimya chenu na kutokufanya kitu… ni dhihaka,” alisema, akiongeza kuwa mashambulizi ya wapiganaji wanaoungwa mkono na Rwanda yanaweza kuleta machafuko zaidi.
“Tatizo hili linaweza kuongeza mgogoro katika kanda nzima ya Maziwa Makuu,” alisisitiza.
Katika hatua nyingine, wapiganaji wa M23 wakiwa na msaada wa Rwanda, walifanya mashambulizi ya upande mwingine na kuteka wilaya mbili za Kivu Kusini baada ya kulishinda jeshi la Congo katika mji mkuu wa Kivu Kaskazini. Jeshi la Congo halikutoa taarifa rasmi kuhusu mashambulizi mapya hayo.
Baada ya mapigano makali yaliyopelekea vifo vya zaidi ya watu 100 na majeruhi karibu 1000, hali ilitulia Goma Jumatano hii, ambapo wakazi walianza kutoka majumbani kwao.
Jean de Dieu, mkaazi wa Goma, alisema kwa simu kutoka mji huo, “Leo hatuogopi,” huku akiongeza kuwa, “Kuna njaa Goma, lazima tuende kuchota maji kutoka ziwani na hatuna dawa.”
Licha ya shinikizo la kimataifa kutaka kumaliza mgogoro huu, Rais Tshisekedi alikataa kushiriki katika mazungumzo ya dharura na Rais wa Rwanda, Paul Kagame.
Hata hivyo, viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walitoa wito wa suluhu ya amani kwa mgogoro huu, wakisisitiza umuhimu wa “serikali ya Congo kushirikiana na wadau wote, ikiwa ni pamoja na M23 na makundi mengine ya silaha.”

Angola, ambayo iliingilia kati kushawishi mazungumzo mapema mwezi jana kabla ya M23 kuanzisha shambulizi, iliwataka viongozi wa Congo na Rwanda kukutana haraka mjini Luanda.
Tshisekedi aliwasili huko kwa mazungumzo kuhusu hatua zijazo.
Mapigano ya hivi karibuni yameongeza janga la kibinadamu, ambapo upungufu wa chakula na maji umeongezeka, na zaidi ya nusu milioni ya watu wamelazimika kuhamia maeneo mengine. Umoja wa Mataifa umetangaza hali hii kuwa ni dharura kubwa.
Katika jiji la Goma, baadhi ya wanajeshi wa Congo walikimbia au walikamatwa, huku maeneo mengi yakikaliwa na wapiganaji wa M23 au wanajeshi wa Rwanda. Hali ya usalama ilizidi kudorora na wizi ulikuwa ukishuhudiwa kwa wingi.



