Shinyanga washauriwa kuweka bajeti posho wenyeviti wa vijiji

HALMASHAURI ya Wilaya ya Shinyanga imeshauriwa katika Mpango wa Rasimu ya Makadirio ya Bajeti ya mwaka 2025/2026 waweke posho za wenyeviti wa vijiji 126 ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kusimamia ukusanyaji wa mapato.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro katika kikao cha baraza la madiwani baada ya Ofisa Mipango wa Halmashauri hiyo Mathew Kayanda kusoma Makadirio ya bajeti ya zaidi ya shilingi Bilioni 44.9.
Mtatiro amesema upo uwezekano wa kuwatengea wenyeviti wa vijiji bajeti hata kidogo kwaajili ya kuwalipa posho itakayo watia moyo wa kusimamia vyema mapato wanayoyakusanya na kubuni vyanzo katika maeneo waliyopo.
“Tumewachagua viongozi wetu wa vijiji nakuwapa dhamana ya kusimamia miradi na Mapato sasa tunaweza kuangalia hata shilingi 20,000 kwa mwezi nao wanufaike na kile wanachokikusanya”alisema Mtatiro.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Ngasa Mboje ambaye ni diwani wa kata ya Mwalukwa amesema mambo yote yanatekelezeka kwani ukichukua idadi ya wenyeviti waliopo ukiwalipa haizidi milioni 30 isitoshe chanzo kingine cha madini ya almas kimeibuka kinaweza kuongeza mapato katika halmashauri.
“Ofisa mipango tuliangalie hili kama linauwezekano kwa kuanza kuwalipa posho kidogo kidogo na pindi mambo yakienda vizuri kiwango kitaongezeka”amesema Ngasa.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Shinyanga vijijini Edward Ngelela amempongeza Mkuu wa wilaya kwa kufanya kazi kubwa ya kushauri huku akiwataka madiwani waichakate bajeti hiyo kwa umakini.
Ofisa Mipango wa Halmashauri hiyo Mathew Kayanda amesema watakwenda kuliangalia suala hilo kama lilivyoelezwa.



