BoT yanunua tani mbili za dhahabu

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imenunua zaidi ya tani mbili za dhahabu ya Tanzania tangu Julai mwaka jana ikiwa ni hatua ya kutimiza lengo lake la kununua tani sita ya dhahabu hiyo kila mwaka.

Mchambuzi wa Masuala ya Fedha wa BoT, Dunga Nginilla alisema hayo mkoani Mtwara akiwasilisha mada ya umuhimu wa dhahabu kama sehemu ya akiba ya fedha za kigeni nchini katika warsha kwa wanahabari mkoani humo.

Nginilla alisema BoT awali ilikuwa na programu ya kununua dhahabu ya Tanzania na kuiweka kama akiba na kuwa mfumo uliokuwa ukitumika kipindi hicho ulikuwa na changamoto.

Alisema mfumo ununuzi huo ulianza tena Oktoba mwaka jana na hadi sasa dhahabu zaidi ya tani mbili kutoka kwa wachimbaji na wauzaji nchini imenunuliwa.

“Lengo la BoT ni kununua dhahabu ya Tanzania tani sita kwa mwaka, tumeanza Julai mwaka jana hadi sasa tumenunua tani zaidi ya mbili,” alisema Nginilla.

Alisema dhahabu ni fedha na imepitishwa kimataifa kuwa nchi ikiwa na akiba ya dhahabu iliyosafishwa kwa asilimia 99.5 inahesabika hiyo ni akiba ya fedha za kigeni.

Alisema mpango huo wa ununuzi wa dhahabu wa BoT una malengo matatu likiwamo la kuongeza akiba ya dhahabu nchini, kutofautisha akiba za fedha na kukuza sekta ya uchimbaji madini ya ndani.

“BoT inanunua dhahabu ya Tanzania tu, wachimbaji au wafanyabiashara wenye vibali na leseni wakitaka kuuza kwetu tunawapa punguzo la mrabaha kutoka asilimia sita hadi nne,” alisema Nginilla.

Alisema kwa sasa wachimbali wengi wa dhahabu nchini wanauza madini hayo BoT na hata wafanyabiashara kwa sababu ya faida wanazopata ikiwamo motisha uliotajwa, lakini pia malipo yao hutolewa ndani ya saa 24 tangu biashara imefanywa.

Alisema katika ununuzi huo hata kampuni kubwa za madini ikiwamo Barrick na nyingine wanawauzia BoT dhahabu kutokana na mfumo rafiki na manufaa wanayopata ukilinganisha na mchakato wa kwenda kuyauza nje wenyewe.

Alisema kwa mujibu wa kifungu cha 59 cha Sheria ya Madini, BoT ina haki ya kununua asilimia 20 au zaidi ya dhahabu ya Tanzania inayotaka kwenda kuuzwa nje hivyo wale wanaouza dhahabu nje wanapaswa kuiuzia BoT asilimia 20 au zaidi ya dhahabu wanayotaka kwenye kuuza nje.

Tanzania ni nchi ya nne barani Afrika kwa uzalishaji wa dhahabu na ya 18 duniani na takwimu zinaonesha uzalishaji utaendelea kukua kuanzia mwaka 2023 hadi 2027.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button