JKCI yawa kimbilio tiba, darasa Afrika
TAASISI ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) imesema imekuwa mfano wa tiba ya moyo Afrika.
Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk Peter Kisenge amesema hatua hiyo ni miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana ndani ya miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.
“Nchi mbalimbali zinakuja kujifunza, hivi karibuni wamekuja watu kutoka Rwanda, Congo (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na hivi karibuni Burkina Faso wamekuja kuona nini Jakaya Kikwete inafanya… na pia wameomba kuleta wagonjwa wao wahudumiwe katika taasisi hii,” alisema Dk Kisenge.
Aliwaeleza waandishi wa habari jijini Dodoma kuwa JKCI imekuwa taasisi kubwa Afrika Mashariki na Kati lakini pia, ni ya tatu kati ya taasisi kubwa za tiba ya moyo zinazomilikiwa na serikali.
Alisema taasisi hiyo imekuwa kubwa kwenye kutoa tiba ya moyo chini ya Rais Samia taasisi imeona wagonjwa 745,837, watu wazima 674,653 na watoto 71,184, wagonjwa waliolazwa 30,643, watu wazima 25,273 na watoto 5372.
“Namba hizi maana yake hakuna taasisi yoyote inayotibu tiba na upasuaji wa moyo inaweza kuona wagonjwa wengi kama hivyo, sisi ndio tunaongoza Afrika Mashariki na Kati na hii ni sababu ya uwekezji mkubwa unafaonywa na Rais Samia,” alisema.
Akitoa mchanganuo, Dk Kisenge alisema wagonjwa waliotibiwa JKCI Upanga ni 513,484 kati ya hao watu wazima 470,119 na watoto 43,365, wagonjwa waliolazwa walikuwa 17,668 watu wazima wakiwa 14,580 na watoto 3,088.
“Katika hospitali yetu ya Dar Group iliyopo eneo la Tazara tumetibu wagonjwa 278,839 kati yao watu wazima walikuwa 238,570 na watoto 40,269. Waliolazwa walikuwa 12,977, watu wazima 10,693 na watoto 2,284,” alisema.
Amesema huduma walizotoa ni za matibabu ya moyo, kinywa na meno, huduma za dharura, kliniki ya wanawake na wajawazito, kliniki ya watoto, macho, pua, masikio na koo, kliniki ya ngozi, vibofu vya mkojo, upasuaji mkubwa na mdogo, magonjwa ya tumbo na ini, figo na matibabu mengine ya magonjwa yanayoambukiza kama malaria.



