Mradi wa bil 36/- kufikisha maji vijiji 37

MRADI wa maji wa Tanga – Horohoro unatarajiwa kuhudumia wananchi takribani 57,334 kwenye kata 10 katika vijiji 37 mkoani Tanga.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mwajuma Waziri alimweleza hayo Rais Samia Suluhu Hassan kabla ya kuweka jiwe la msingi la mradi huo wilayani Mkinga.

Mwajuma alisema serikali inatekeleza mradi huo unaogharimu Sh bilioni 35.7 kwa kuwa kuna changamoto katika vijiji vingi vilivyopo kwenye mwambao wa bahari.

“Hivi vijiji vya mwambao huu wa bahari changamoto ya maji chini ya ardhi yana chumvi, hiyo changamoto imepelekea katika Serikali ya Awamu ya Sita kusanifu mradi huu ambao unagharimu takribani Shilingi bilioni 35.7 ambayo ulitupa Rais ili kuutekeleza,” alisema.

Mwajuma alisema hadi sasa serikali imelipa Sh bilioni 11 kati ya Sh bilioni 35 na utekelezaji wake umefikia asilimia 46 na mwisho wa utekelezaji wa mradi huo ni Oktoba, mwaka huu.

Alisema urefu wa bomba lote ni kilometa 91.9 na mpaka sasa mkandarasi amepeleka yenye urefu wa kilometa 37 na amelaza kilometa 15 na njia ya usambazaji inatarajiwa kuwa kilometa 104.

Kwa mujibu wa Mwajuma, wanatarajia wananchi wa eneo la Mtimbwani muda si mrefu wataanza kupata huduma ya maji na baada ya hapo yatafikishwa Kibibioni ambako kuna tangi.

“Doda kuna tangi na hapa tulipo panaitwa Manza ambako kuna kituo cha kuyaongeza nguvu. Haya maji yataishia hapa kwenda kwa mserereko, baada ya hapo itabidi tuyapampu kuyapeleka eneo la Parungukasera ambako tutajenga tenki tena la ukubwa wa meta za ujazo 500,000 na baada ya hapo tutayapampu kuyapeleka Kiluluduga,” alisema Waziri.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button