Viongozi wa CCM Kigoma wakwazwa ukarabati MV Liemba

Kamati ya siasa ya halmashauri kuu ya CCM mkoa Kigoma imesikitishwa na kuchelewa kuanza kwa ukarabati mkubwa wa meli ya Mv Liemba kwa zaidi ya miezi sita sasa hivyo imetoa maelekezo kuhakikisha ukarabati huo unaanza haraka.
 
Mwenyekiti wa CCM mkoa Kigoma, Jamal Tamim alitoa maelekezo hayo wakati kamati hiyo ilipofanyika ziara katika bandari ya Kigoma kutembelea na kukagua maendeeo ya ukarabati wa meli hiyo ya abiria na mizigo na meli yya mafuta ya MT Sangara.
 
Tamim amesema taarifa ya wasimamizi wa mradi huo Kampuni ya meli Tanzania (TASHICO) kuonyesha ukarabati huo umefanyika kwa asilimia 10 tangu mwezi Julai mwaka jana zinatia simanzi kwani nguvu kubwa waliyokuwa wanatumia kuwaeleza wananchi kuwa ukarabati huo utafanyika na kumaliza haraka na meli itaanza kutoa huduma muda si mrefu unawafanya kuonekana waongo kwa wananchi.
 
Kwa upande wake Mbunge wa Kigoma Mjini, Kilumbe Ng’enda amesema jambo la kusikitisha ni kwamba wanaosimamia ukarabati huo wanaeleza tatizo ni chelezo lakini baada ya chelezo kukarabatiwa na kuanza kutoa huduma zimekuwa zikipandishwa meli nyingine za watu binafsi na meli hiyo ikiwa imeachwa pembeni kwa muda mrefu bila kufuata muda wa mkataba wa ukarabati wa meli hiyo.
Awali Meneja wa TASHICO tawi la Kigoma, Humphrey Mwambungu amedai tayari ukarabati wa meli hiyo umeanza kwa kuondoa injini na mashine zilizopo ndani ya meli ili kuweka mpya na kwamba muda si mrefu itapandishwa kwenye chelezo ili kufanyiwa ukarabati wa nje sambamba na ukarabati wa ndani kuendelea.
 
Mwambungu amesema awali meli ya MT Sangara ndiyo ilikuwa inakarabatiwa ikiwa juu ya chelezo na tayari imeshashushwa ikiendelea na umaliziaji ikiwa imefikia asilimia 98 na kwamba muda mfupi ujao meli ya MV Liemba yenye mkataba wa miezi 24 ya ukarabati mkubwa itapandishwa kwenye chelezo ili kuanza kufanyiwa ukarabati huo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button