Mloganzila yapendekezwa kuitwa Ali Hassan Mwinyi

ALIYEKUWA Makamu Mkuu wa Kwanza wa Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Profesa Kisali Pallangyo amependekeza Hospitali ya Mloganzila iitwe Kituo cha Matibabu cha Ali Hassan Mwinyi kuakisi mchango wake alioutoa katika maendeleo ya chuo hicho na sekta ya afya.

Aliyasema hayo jana wakati akieleza mchango wa hayati Mwinyi ambaye alikuwa Mkuu wa chuo hicho wa kwanza kutoka mwaka 2007 hadi 2024 na Rais wa Serikali ya Awamu ya Pili.

Profesa Pallangyo alisema, Mwinyi alishiriki upatikanaji wa eneo la Mloganzila mwaka 2006 na kuliendeleza hadi kujenga hospitali hiyo na Kituo cha Magonjwa ya Moyo Afrika Mashariki.

Alisema ujenzi wa hospitali hiyo ni kuwezesha wanafunzi wa tiba chuoni hapo kupata mafunzo kwa vitendo kuwawezesha kuwa bora wanapokwenda kuhudumia jamii katika zahanati, vituo vya afya na hospitali.

“Lengo la Mwinyi lilikuwa ni kuimarisha miundombinu ya kujifunzia na kuongeza ubora wa ujifunzaji. Kwa usimamizi wake katika miaka 15, alitusaidia kufikia hapa, napendekeza jina la hospitali libadilishwe ikiwapendeza,’’ alisema Profesa Pallangyo.

Akielezea mafanikio ya hayati Mwinyi, alisema aliwezesha kuimarisha ubora wa ufundishaji, kuongeza tafiti na ushirikiano wa kimataifa na kutoa mafunzo ya utafiti kwa wafanyakazi na wanafunzi.

Alifafanua kuwa udahili wa wanafunzi wa shahada uliongezeka kutoka 310 mwaka 2007 hadi 856 mwaka 2024, wanafunzi wa uzamili na uzamivu waliongezeka kutoka 168 hadi 985. Pia, miradi ya utafiti imeongezeka kutoka 57 hadi 148.

“Katika uongozi wake, alifanya kazi kwa uadilifu na wala hakuwa na makuu kwa sababu katika miaka yote 15 hakuwahi hata siku moja kuacha kuja kwenye mahafali kuhudhurisha wahitimu,” alisema.

Alifafanua katika kipindi hicho, MUHAS imeweza kuchochea mabadiliko ya sekta ya afya kwa kuongeza idadi ya wataalamu wa sekta ya afya, kuchangia upatikanaji wa miongozo ya kudhibiti na kukabiliana na magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza.

Pia, alisema kuwa na wataalamu wabobezi katika magonjwa ya moyo, figo, ini ambao wamewezesha kupunguza idadi ya Watanzania wanaokwenda nje ya nchi kupata matibabu ya magonjwa hayo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button