Msigwa aanika mafanikio lukuki mkutano wa kahawa

MSEMAJI Mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa amesema mkutano wa tatu wa nchi zinazozalisha kahawa Afrika uliofanyika hivi karibuni nchini, umeleta manufaa mengi kwa nchi.
Msigwa alisema hayo jana Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mambo mbalimbali, ikiwemo ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan mkoani Tanga.
Alisema kupitia mkutano huo Tanzania ilipata nafasi ya kujitangaza zaidi katika ramani ya wazalisha kahawa duniani kama nchi iliyofanikiwa kulifanya zao hilo kuwa la kimkakati kupitia nafasi yake ya uenyeji.
“Hili lilikuwa jambo muhimu kwa sababu tulihitaji kupeleka ujumbe duniani kama sisi ni wazalishaji wa kahawa, kwenye safari yetu ya kwenda kufikia uzalishaji wa tani 300,000 ni lazima dunia ijue ili tuongeze wigo wa watu wanaotaka kuja kununua kahawa kutoka hapa Tanzania’’ alisema.
Alisema kupitia mkutano huo ulioandaliwa na Shirika la Kahawa Afrika (IACO), shirika hilo liliahidi kuleta miradi mingi inayohusiana na kahawa nchini, ikiwemo ujenzi wa Kituo cha utafiti wa kahawa Afrika kitakachojengwa mkoani Kilimanjro eneo la Lyamungo ambako kuna Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania (TaCRI).
“Pia, limeahidi kujenga kituo cha umahiri Dodoma kitakachotumika kutoa elimu, kujengea uwezo wataalamu na kuhamasisha uongezaji thamani na kutoa taarifa za mnyororo wa thamani wa zao la kahawa,’’ alisema.
Akizungumzia jitihada zinazofanywa na nchi katika kuongeza thamani ya zao la kahawa, Msigwa alisema viwanda 28 vya kukoboa kahawa vinavyomilikiwa na sekta binafsi, serikali na vyama vya ushirika vimejengwa.
Pia, alisema viwanda viwili vya kuongeza thamani vimejengwa sambamba na viwanda vingine 37 vya kukaanga kahawa vimejengwa.
Vilevile, alisema serikali imedhamiria kuongeza matumizi ya kahawa inayozalishwa nchini kutoka asilimia saba za sasa hadi asilimia 15 kwa kuhamasisha ufunguaji wa migahawa ya kisasa, kutoa mafunzo kwa wahudumu wa migahawa mikubwa na hoteli, wauzaji wa mitaani na kuanziasha migahawa inayotembea kwa kutumia pikipiki za magurudumu matatu.
Akizungumzia kuhusu ziara ya Rais Samia mkoani Tanga, Msigwa alisema kuwa ziara hiyo imefanikiwa kwa asilimia 100.
Alisema idadi ya wahudhuriaji mikutano, wingi wa miradi iliyokaguliwa na tathmini iliyofanywa imeonesha kuwa ziara hiyo imefanikiwa.
Akiwa mkoani Tanga, Rais Samia alitembelea miradi kadhaa, ikiwemo mradi wa ujenzi wa Bwawa la Mkomazi unaotekelezwa kwa ruzuku ya serikali na unagharimu Sh bilioni 18.2 ambao umefikia asilimia 35 na utakapokamilika utawanufaisha wakulima zaidi ya 20,000 kutoka vijiji 28 na kata saba.



