JKCI kupima moyo wajawazito, watoto Arusha

TAASISI ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) imeandaa huduma za upimaji wa magonjwa ya moyo bure kwa wanawake, wajawazito na watoto mkoani Arusha.
Taarifa ya Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano JKCI, Anna Nkinda imeeleza kuwa huduma hiyo itatolewa katika viwanja vya TBA Kaloleni jirani na mnara wa mwenge.
“Upimaji huu utafanyika bila malipo yoyote ambapo wataalamu wanawake wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete watatoa huduma hii Machi Mosi hadi 8, mwaka huu saa 2:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni,” ilisema taarifa hiyo.
Nkinda alieleza kuwa pia kutakuwa na wataalamu wa lishe watakaotoa elimu ya lishe bora kwa wananchi kuwapa uelewa wa kuzingatia mtindo wa maisha ili kuepuka magonjwa ya moyo.
Kambi hiyo ya utoaji wa huduma hizo inatolewa kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha.
Nkinda alieleza kuwa uchunguzi wa kina utafanyika na watakaobainika na magonjwa watatibiwa papo hapo na wenye uhitaji wa matibabu ya kibingwa watapewa rufaa ya kutibiwa JKCI Upanga mkoani Dar es Salaam.
Wakati huohuo, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Jumanne Sagini ameupongeza uongozi wa Mkoa wa Arusha kwa maandalizi mazuri ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.
Sagini alisema hayo mwishoni mwa wiki jijini Arusha alipotembelea mabanda yanayotoa huduma za msaada wa kisheria kupitia kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia.
“Nawapongeza viongozi wa mkoa, mkurugenzi na timu nzima kwa jinsi walivyojipanga kuhakikisha huduma hizi muhimu za msaada wa kisheria zinatolewa kwa ufanisi,” alisema.
Sagini alihimiza wakazi wa Arusha kujitokeza kwa wingi kupata msaada wa kisheria kwa kuwa kuna wataalamu kwa ajili ya kuwahudumia, wakiwemo wataalamu kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), jumuiya ya mawakili wa serikali, taasisi za kisheria na mawakili binafsi.
“Nimeona watu wengi wanahitaji huduma za kisheria na jambo la kufurahisha ni kuwa sekta zote muhimu za kisheria zipo hapa kushirikiana ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora,” alisema.
Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani Machi 8, yatafanyika kitaifa mkoani Arusha na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan.



