Bil 2/-zaokolewa kupandikiza figo, uloto
HOSPITALI ya Benjamin Mkapa mkoani Dodoma imeokoa Sh bilioni mbili katika huduma mbili za kibingwa kwa magonjwa ya figo na selimundu kuanzia mwaka 2021 hadi sasa.
Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Profesa Abel Makubi alisema hayo Dodoma jana wakati akieleza mafanikio ya hospitali katika kipindi cha miaka minne na mwelekeo katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Profesa Makubi alisema hospitali hiyo imepandikiza figo wagonjwa 25 kati ya 50 katika kipindi cha miaka minne kwa gharama ya Sh milioni 875.
Alisema kati ya wagonjwa hao 10 wamelipiwa matibabu kupitia Mfuko Maalumu wa Rais Samia Suluhu Hassan Sh
milioni 350.
Profesa Makubi alisema endapo wagonjwa hao wangepelekwa nje ya nchi serikali ingetumia Sh bilioni 1.87 hivyo kiasi cha Sh bilioni moja kimeokolewa.
Makubi alisema hospitali hiyo imeokoa Sh bilioni moja kwa kupandikiza uloto.
Aliwaeleza waandishi wa habari kuwa watoto 20 waliokuwa na ugonjwa wa selimundu walipandikizwa uloto na wamepona.
Alisema huduma hiyo ilitumia Sh bilioni 1.1 iliyotolewa kupitia Mfuko Maalumu wa Rais Samia Suluhu Hassan na kama watoto hao wangepatiwa huduma hiyo nje ya nchi, ingetumika Sh bilioni 2.1 hivyo Sh bilioni moja imeokolewa.
Kwa mujibu wa Profesa Makubi katika kipindi cha miaka minne ya Rais Samia, uvunaji wa figo katika hospitali hiyo umeboreshwa kwa teknolojia ya kisasa kwa kutumia matundu madogo na kupunguza rufaa za kwenda nje ya nchi kwa asilimia 99.
Alisema huduma za kibingwa na ubingwa wa juu zimeongezeka kutoka huduma katika maeneo saba hadi 16 ya ubobezi tangu Serikali ya Awamu ya Sita iingie madarakani mwaka 2021.
“Katika kipindi cha miaka minne BMH imefanya upasuaji wa moyo kwa kufungua kifua kwa wagonjwa 60 kati ya hao watoto 38 na watu wazima 22.
Kiasi cha fedha kilichotumika ni Shilingi milioni 562 kati ya hizo milioni 100 zilitoka Mfuko Maalumu wa Samia Suluhu Hassan,” alisema Profesa Makubi.
Alisema kutokana na umahiri wa wataalamu wa hospitali hiyo, wamefanikiwa kufanya uchunguzi wa mishipa ya moyo kwa wagonjwa 1,173, upandikizaji betri wagonjwa 23, kuweka vizibua njia ya mishipa ya moyo kwa wagonjwa 42.
Vilevile, hospitali hiyo imefanikiwa kuanzisha huduma ya kuweka vipandikizi maalumu kwenye uume.
Alisema wanaume waliokuwa na changamoto za upungufu wa nguvu za kiume wamewekewa, ikiwa ni hospitali ya kwanza kutoa huduma hiyo nchini.
Profesa Makubi alisema tafiti zinaonesha wanaume wengi wanakabiliwa na tatizo la upungufu wa nguvu za kiume na wengi wamefika hospitalini hapo kutafuta huduma ya upandikizaji wa uume.
“Tayari wanaume watano wamefanyiwa upasuaji huo, lakini changamoto kubwa ni gharama zinazofikia Shilingi milioni tano hadi sita,” alisema.
Alisema hospitali hiyo inaendelea kushirikiana na serikali kupunguza gharama za huduma hiyo ili ipatikane kwa wengi.
Aidha, alisema hospitali hiyo inatarajia kuanza kutumia roboti kwa upasuaji ndani ya miaka mitatu ijayo ili kuongeza usahihi wa matibabu.
Imeandikwa na Sifa Lubasi (Dodoma) na Selemani Nzaro (Dar es Salaam)



