Kituo cha afya Kingolwira chahitaji msaada mashuka

KITUO cha Afya Kingolwira kiliyopo Manispaa ya Morogoro kimewaomba wadau kujitokeza kutoa misaada ya aina mbalimbali ikiwemo mashuka na vifaa vya usafi.

Lengo ni kuboresha huduma za afya hususani kwa wanawake wajawazito wanaolazwa na wanaojifungua kwa vile mahitaji bado ni makubwa.

Mwakilishi wa mganga mkuu wa kituo hicho, Dk Hemedi Kiduba ametoa ombi hilo wakati akipokea mashuka na vifaa vya usafi kutoka kwa Kamati ya Wanawake wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) Mkoa wa Morogoro.

Vifaa hivyo vilikabidhiwa kwa wajawazito waliolazwa katika wodi ya wazazi ya kituo hicho.

Wanawake wa tughe mkoa licha ya utoaji misaada katika kituo hicho pia walitoa misaada mingine katika Kituo cha Arise and Shine kilichopo Manispaa ya Morogoro na kinachohudumia watoto wa kike, ikiwa ni shamrashamra za kuelekea kilele cha siku ya wanawake duniani Machi 8, mwaka huu.

Dk Kiduba amesema kituo cha Kingolwira kinaendelea kutoa huduma kwa mama na mtoto, lakini kinakabiliwa na changamoto ya vifaa kama mashuka na vifaa vya usafi bado ni kubwa.

“Tunawashukuru Tughe kwa kujitoa kusaidia akina mama wetu, kwani hii itasaidia kuboresha mazingira ya huduma zetu na msaada huu umekuja kwa wakati muafaka kwani mahitaji ya mashuka na vifaa vya usafi kwa akinamama wanaojifungua ni makubwa,” amesema Dk Kiduba.

Kwa sasa kituo hicho pia kinapokea wagonjwa kutoka kata nyingine za jirani ikiwemo ya Makambalani iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro.

Naye Mwenyekiti wa Tughe Mkoa, Noves Nkwera amesema kuwa utoaji wa misaada hiyo ni sehemu ya dhamira yao ya kusaidia jamii na kuhakikisha kuwa makundi yenye uhitaji yanapata faraja.

“Sisi wanawake wa Tughe tunatambua changamoto zinazowakumba akina mama hospitalini na watoto wanaoishi katika mazingira magumu, na tunaamini kwa kushirikiana tutasaidia kuboresha maisha ya watu katika jamii yetu,” amesema Noves.

Noves alisema anatumaini msaada wao huo utakluwa umeacha  tabasamu kwa waliopokea  na kutoa hamasa kwa wengine kuendeleza moyo wa kusaidiana kwa ajili ya ustawi wa jamii nzima.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti Tughe mkoa  katika Kituo cha Arise and Shine chenye kuleta  watoto wa kike walioko katika mazingira magumu walikabidhi vifaa vya usafi zikiwemo  sabuni  na misaada mingine ikiwemo mafuta ya kupikia, viroba vya michele, sukari na vyakula vya aina mbalimbali.

Kwa upande wake Mlezi wa watoto wa Kituo cha Arise and Shine,Tumaini Pagata aliwashukuru wanawake wa Tughe kutokana na msaada wao kwa  watoto wanaotunzwa na Kituo hicho ambao  wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa vifaa vya usafi hasa katika siku zao za hedhi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button