Sababu za popo kulala kichwa chini miguu juu

POPO ni mnyama mwenye maajabu makuu mawili yaani, kuwa ndiye mnyama pekee duaniani anayeweza kuruka kama ndege pamoja na tabia yake ya kulala akiwa amening’inia kichwa chini migu juu.
Katika makala haya, Mwandishi Wetu anatumia vyanzo mbalimbali kumjadili mnyama huyu. Fuatilia…
Kwa mujibu vyanzo mbalimbali, watu wengi hudhani popo haoni. Chanzo mtandaoni kinasema: ‘Ukweli ni kwamba, anaona vizuri kushinda hata wanyama wanaotembea mchana.’
Kuhusu namna popo anavyoweza kukamata wadudu usiku, kinasema mnyama huyu amejitengenezea aina ya mawimbi ya sauti yanayomsaidia kuwinda, kinasema: ‘‘Njia hii huitwa ‘echolocation’ yaani njia ya ‘kuona’ kwa sauti, ambapo popo wanapiga kelele hadi usiku na kusikiliza mwangwi kwa masikio yao nyeti kuwaambia mawindo yao yapo wapi.”
Chanzo kinaeleza, “Popo ndiye mnyama pekee anayetoa haya mawimbi ya sauti duniani. Cha ajabu ni kuwa, mawimbi ya sauti yanayotolewa na popo ni makubwa sana kushinda sauti zote hapa duniani,” na kuongeza: “… hii sauti ikigonga kitu kiwe mti au mdudu inarudisha taarifa kwenye ubongo wake na kutafsiri na popo anakuwa tayari amejua ni kitu gani hicho na kipo umbali gani.”
Makala yenye kichwa cha habari: ‘Zijue Jamii Mbalimbali za Popo, Tabia, Maisha Yao na Umuhimu Wake Katika Uhifadhi’ yaliyoandaliwa na Ezra Mremi na kuhaririwa na Hillary Mrosso na Alphonce Msigwa (Ofisa Uhifadhi katika Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania) Juni 26, 2023 iliyopo mtandaoni inamwelezea popo ikisema ni wanyama aina ya mamalia mwenye damu moto, miili iliyofunikwa na nywele, anayezaa na kunyonyesha watoto kwa kutumia viwele vyake.
Kibiolojia, makala hayo yanasema: “… wanapatikana katika oda ya kipekee ya chiroptera ikimaanisha wanyama ambao miguu yao ya mbele imekuwa mabawa.”
Kwa mwonekano, mifupa ya miguu ya mbele ya popo inafanana na mikono ya binadamu, ikiwa na mifupa mirefu minne mithili ya vidole iliyofunikwa na ngozi nyembamba.
Makala yameandika: ‘Mfupa mmoja umejitenga mithili ya dole gumba lenye kucha ambao hutumika kushikilia chakula, kujihami au kutambaa.’
Popo huishi katika mapango, misitu au kwenye majengo, madaraja, minara na kadhalika. Jamii za popo zimegawanyika katika makundi makuu manne, yaani popo wala wadudu, wavuvi, wala matunda na popo wanyonya
damu.
Popo wanyonya damu huishi kwa kunyonya damu kwa wanyama wa aina mbalimbali. Popo wana mbawa nyepesi zinazorahisisha kuruka haraka na kubadilisha mwelekeo na huzitumia kukamata mawindo. Wanatajwa kama wanyama wenye mifumo ya ajabu ya kinga na kwamba wana uwezo wa kula hadi mbu 1,200 kwa saa.
Chanzo kinasema, ‘‘Pua zao zinaweza pia, kutambua kama kiumbe chenye damu moto kipo karibu ambazo husaidiana na masikio. “Masikio yao huweza kusikia sauti za mnyama anayepumua akiwa amelala au ametulia, ili kuweza kwenda kunyonya damu.”
Kwa mujibu wa tafiti za kitaalamu, mate ya popo hao husababisha ganzi kwa mnyama pindi wanapolamba damu na
kusababisha mnyama huyo kutohisi maumivu na pia, mate hayo huzuia jeraha kuvimba. Jamii nyingine ni popo
wavuvi. Miguu ya popo hawa ina vidole vyenye kucha ndefu zenye nguvu ambazo huziingiza ndani ya maji na kutoa windo lake hususani samaki.
Wengine ni popo wala matunda; hawa wana macho makubwa yanayoona vyema kwenye giza au mwanga mdogo,
lakini hayaoni vizuri kwenye mwanga mkali, hivyo kuwafanya wafanye shughuli zao usiku zaidi.
“Pua zao zinaweza kunusa vyema kama zilivyo za mbwa wa nyumbani, na kuwafanya waweze kufanikiwa kujua kilipo
chakula,” wanasema wataalamu hao katika chapisho lao mtandaoni.
Faida za popo
Chapisho la Zijue Jamii Mbalimbali za Popo, Tabia, Maisha Yao na Umuhimu Wake Katika Uhifadhi’ linaandika,
“Popo hawa wana faida nyingi, ikiwamo kuchavusha mimea mbalimbali pale wanapotafuta chakula kwenye maua na kusambaza chavua, pia wanapokula matunda husambaza mbegu zinazotoka kwenye kinyesi chao.”
Linaongeza: “Mbali na faida, popo hawa wanaonekana kama waharibifu miongoni mwa wakulima wa matunda.”
Inaaminika kuwa, popo wana uwezo mkubwa wa kubeba magonjwa yanayoweza kuathiri binadamu na wanyama jamii ya nyani/ngedere yakiwamo magonjwa ya ‘ebola’ na ‘marburg’ endapo watadondosha vinyesi au mate kwenye matunda au mboga zinazoliwa na binadamu au kama popo watafanywa kitoweo.
Sababu za popo kuning’inia Kwa mujibu wa chapisho hilo, zipo sababu nyingi za popo kuning’inia kichwa chini, miguu juu hata anapokuwa amelala. Linasema kwa kawaida viumbe wengi wakining’iniza kichwa chini hata kwa muda mfupi tu damu hukimbilia kwenye ubongo na kusababisha kizunguzungu.
“Hali haiko hivyo kwa popo kwani huweza kuning’inia hata kwa miezi kadhaa bila tatizo… “Hupenda kuning’inia
sehemu ambazo zina giza au kivuli ambapo si rahisi maadui kuwapata,” linabainisha. Chapisho hilo na vyanzo
vingine libainisha sababu kuu za popo kuning’inia kuwa ni pamoja na udogo wa miili yao pia, wana uzito mdogo na kiasi kidogo cha damu.
Inaelezwa kuwa, uzito mdogo huchangia kupunguza nguvu za uvutano ambazo husababisha damu kurudi kichwani kwa wingi kwa mnyama mwenye uzito mkubwa anaponing’inia kichwa chini na miguu juu. Uimara wa mifupa ya nyonga nao unatajwa kuwa kichocheo na sababu ya tabia ya popo kuning’inia na hata kulala kichwa chini miguu juu.
“Ukitoa jamii ya popo wanyonya damu, jamii nyingine zina mifupa midogo na isiyo na nguvu ya nyonga na ya miguu ya nyuma,” kinasema chanzo.
Kinaongeza: “Mifupa hii huwasaidia viumbe warukao kama ndege kuanza kuruka kutokea ardhini kwa kukimbia ndipo wapae au kurusha mwili juu kabla ya kuanza kutumia mabawa. “Popo akining’inia kutumia miguu humsaidia pindi anapotaka kuruka kwani hufanya kujiachia tu na kuendelea kupaa.”
Kuhusu muundo wa maungo yake, vyanzo mbalimbali vinasema maungio ya magoti ya popo yanaelekea nyuma, na pia vidole vya miguu yake vimeundwa na misuli imara. Kimoja kinasema, “Popo wakining’inia hawatumii nguvu
yoyote na badala yake huwa ni kama wamelegeza misuli ya miguu ambayo huvifunga viungo vya miguu kukaza sehemu waliposhikilia.”
Kinasema hali hii humwezesha popo kuning’inia kwa urahisi hadi miezi kadhaa na hata wakifa huendelea kuning’inia. Kujikinga dhidi ya maadui pia, kunatajwa kuwa ni moja ya sababu za popo wengi kuning’inia sehemu zenye giza ambazo si rahisi adui kufika wala kuwaona.
“Popo pia, huweka mpango wa kukimbia haraka endapo adui atagundua sehemu walipo na huifanya kazi hii kwa kujiachia tu,” kinasema chanzo na kuongeza kuwa, “Popo wanapolala hutumia mabawa yao kujifunika ili
kujikinga dhidi ya baridi au mvua.
“Ni ngumu kwa popo kujifunika vyema kama atakuwa yupoardhini”.



