G-25 na thamani ya kahawa Afrika

KWA kutazama kijuu juu unaweza kudhani zao la kahawa ni la kawaida na pengine halina faida au kipato chake ni kidogo na pengine ni zao la watu wa hali ya chini.

Kwa Tanzania imezoeleka kuona wauza kahawa wakipita barabarani na chombo maalumu kilicho juu ya moto wa mkaa na vikombe vidogo na kashata.

Mitaani pia kuna vijiwe vya kahawa, watu hukusanyika na mara nyingi huwa ni wanaume hususani nyakati za asubuhi na jioni wakizungumza haya na haya hususani masuala ya siasa na michezo. Hili ni zao ambalo mzizi wake ni Afrika, lakini cha ajabu faida wanapata watu wa nchi za Ulaya na Afrika wanabaki kuambulia patupu!

Tanzania ni nchi ya nne kwa uzalishaji kahawa Afrika baada ya Ethiopia ambayo ni ya kwanza ikifuatiwa na Ivory Coast na Uganda. Nchi nyingine zinazozalisha kahawa kwa wingi Afrika ni Kenya, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Malawi, Cameroon, Zimbabwe, Madagascar, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Zimbabwe.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, nchi nyingine ni Angola, Ghana, Guinea, Sierra Leone, Togo, Afrika Kusini, Algeria, Benin, Gabon, Equatorial Guinea, Liberia na Nigeria.

Februari 21 na 22, Tanzania ilipata ugeni wa marais na mawaziri kutoka nchi 25 zinazozalisha kahawa Afrika waliohudhuria Mkutano wa Tatu wa G-25.

Mkutano huo ulitokana na azimio la kuhakikisha kahawa inapandishwa thamani huku ikitoa ajira kwa vijana na wanawake. “Kahawa inachangamsha…!” anasema Rais Samia Suluhu Hassan na kuomba kupewa kikombe cha kahawa anywe kabla ya kuanza kuhutubia marais, mawaziri na wageni mbalimbali waliofika nchini kushiriki mkutano huo.

Katika hotuba yake, Rais Samia anasema Afrika lazima ifanye jitihada kubwa kuongeza uzalishaji na thamani ya zao la kahawa mpaka kufikia mwaka 2035 kwani inaumiza kuona kahawa inalimwa Afrika lakini, bara hilo halifaidiki.

Katika kuchagiza safari hiyo, Samia anasema Tanzania ilishaanza harakati za kulithaminisha zao hilo kupitia mradi wa Jenga Kesho iliyo Bora (BBT) na kwamba, iko tayari kufundisha nchi nyingine ili vijana wa Afrika wapate ajira.

“Na si kahawa tu, BBT inaelekeza pia kilimo cha mazao mengine ya biashara, ufugaji na uvuvi. Kwa sasa nchini Tanzania kila zao ni zao la biashara kwa hiyo tupo tayari kufundisha nchi nyingine kama zinahitaji,” anasema.

Rais Samia Suluhu Hassan akiwa na viongozi mbalimbali walioshiriki Mkutano wa Tatu wa Nchi zinazozalisha Kahawa Afrika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam hivi karibuni.

“Kwa Tanzania tumepanga mpaka ikifika mwaka 2030, asilimia 20 hadi 25 ya kahawa tunayozalisha ifanyiwe uchakataji hapahapa nchini,” anasema. Uchakataji kahawa ndio tatizo kubwa linalozikabili nchi za Afrika na kulazimika kuuza kahawa ghafi nje na kisha kuuziwa kahawa iliyochakatwa kwa bei kubwa.

Takwimu zinaonesha kuwa, Afrika inauza kahawa ghafi yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni tatu na kuagiza kahawa yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 50. “Kahawa ya Afrika imekuwa haina thamani kwani inauzwa nje ikiwa ghafi kwa fedha kidogo kisha inanunuliwa tena kwa fedha nyingi hali inayofanya ikose thamani na watu wake kuendelea kuwa masikini,” anasema Rais Samia.

Anasema takwimu zote zinaonesha kila siku watu wanakunywa vikombe takribani bilioni 3 vya kahawa dunia nzima na kati ya hivyo, kahawa nzuri ni ya Afrika lakini kumekuwa na changamoto nyingi ambazo viongozi wa serikali za Afrika wanatakiwa kuzifanyia kazi kuzitatua.

“Miaka ya 1960 uzalishaji kahawa ilikuwa asilimia 25, lakini sasa uzalishaji umeshuka na kufikia asilimia 11 ya kahawa yote inayozalishwa duniani licha ya soko la kahawa kuwa kubwa duniani… Manufaa na fursa tunazopata kulinganisha na nchi nyingine duniani pia yameshuka,” anasema.

Katika mnyororo wa thamani ya kahawa duniani unaokadiriwa kufikia thamani ya Dola za Marekani bilioni 500, Afrika inaambulia asilimia 0.3. “Zaidi ya asilimia 90 ya mapato yanayopatikana na kahawa inayozalishwa katika Bara la Afrika inakwenda nje, wazalishaji ni sisi lakini faida inakwenda kwingine Afrika tunabaki kama shamba tu,” alieleza.

“Inabidi tuitazame vizuri kama Waafrika na tubadilike, changamoto hii ya kimkakati sioni namna inavyoweza kutatuliwa bila jitihada zetu wenyewe,” anasema Rais Samia. Katika Azimio la Dar es Salaam, moja ya mambo ambayo nchi hizo ziliazimia ni kushirikiana kufanya tafiti na kuongeza thamani ya kahawa ili kupata mavuno bora na kukuza uchumi wa Afrika.

Nchi hizo zimeomba Umoja wa Afrika (AU), kushirikisha Shirika la Kahawa Afrika (IACO) zinapokuwa zinajadili masuala ya kahawa na Umoja wa Ulaya (EU) na kutofanya uamuzi bila kuishirikisha Afrika. Akisoma azimio hilo, Waziri wa Kilimo Hussein Bashe anasema mengine waliyokubaliana ni kusaidiana katika uwekezaji ili kuongeza thamani ya kahawa na kukuza matumizi ya ndani ya bidhaa hiyo.

“Pia tumeazimia kuchakata na kufanya biashara ya kahawa angalau asilimia 50 ndani ya Bara la Afrika ifikapo mwaka 2035, na kubuni mbinu mpya za kiteknolojia katika mnyororo wa thamani wa kahawa,” anasema Bashe.

Kuhusu matakwa yao mbali na kutaka AU iishirikishe IACO kwenye uamuzi unaohusu kahawa katika nchi za Ulaya, pia wametaka kuanzishwa viwanda vya kuchakata kahawa kwa nchi hizo na kuwepo kwa kituo cha utafiti wa zao hilo Afrika.

“Serikali za Afrika, ziunge mkono juhudi za kuongeza matumizi ya kahawa ya ndani, lakini pia ziwezeshe raia wao kuwekeza katika sekta binafsi ili kulipa thamani zao la kahawa,” anasema Bashe. Baadhi ya viongozi wanazungumzia azimio hilo na kusema yote waliyoazimia hayapingiki, bali yanapaswa kuzingatiwa kwa ustawi wa Afrika.

Mwenyekiti wa IACO na Waziri wa Kilimo na Mifugo wa Burundi, Prosper Dodiko anasema Burundi inatambua umuhimu wa azimio hilo na iko tayari kulitekeleza kwani zao la kahawa lina mchango mkubwa katika kukuza uchumi ama uwe wa mtu binafsi, kitaifa na hata kimataifa.

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), Primus Kimaryo, anasema Tanzania inaungana na wazalishaji wengine kuleta mapinduzi ya kahawa barani Afrika ili thamani ya zao hilo muhimu kiuchumi ipande sambamba na kutoa ajira kwa vijana na wanawake.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya kahawa ya Amir Hamza Ltd inayozalisha kahawa ya Amimza, Amir Hamza ambaye amekuwa katika sekta ya kahawa kwa miaka 30, anampongeza Rais Samia kwa kuruhusu mkutano huo kufanyika nchini kwani manufaa yake ni makubwa.

“Mkutano wa kwanza ulikuwa Kenya, wa pili Uganda na huu ni wa tatu nchini Tanzania. Mimi mdau wa kahawa naona kwa maazimio haya, kahawa itapiga hatua kubwa na siku si nyingi tutakuwa na viwanda vyetu wenyewe vya kuchakata kahawa,” anasema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button