ATHARI ZA FUNZA MWEKUNDU: Zuio kilimo cha pamba si adhabu

KILIMO cha pamba ni sekta muhimu kwa uchumi wa wakulima na taifa kwa ujumla.

Hata hivyo, mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma, Njombe, Songwe, Rukwa na Mbeya imewekewa zuio la kulima pamba kutokana na uwepo wa funza mwekundu.

Huyu ni mdudu hatari anayesababisha uharibifu mkubwa katika zao la pamba na kusababisha hasara kwa wakulima. Serikali imeweka zuio la kilimo cha pamba katika mikoa hiyo kuzuia kuenea kwa mdudu huyu katika ukanda wa uzalishaji pamba waMagharibi na Mashariki ambako pamba ni zao tegemeo la biashara.

Taarifa za vyanzo mbalimbali zinasema udhibiti wa mdudu huyo unahitaji matumizi makubwa ya viuadudu. Jambo hili lhusababisha changamoto kwa wakulima, mazingira na hata soko la kimataifa la pamba.

Mtafiti wa Entomolojia (utafiti wa wadudu) wa Pamba katika Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Dk Abdullah Mkiga, anasema funza mwekundu ana tabia ya kuingia kwenye pamba na kushambulia sehemu muhimu.

Kwamba, hali hiyo husababisha uharibifu mkubwa kwenye pamba kabla ya kuvunwa. Anasema funza mwekundu anapotaga mayai kwenye maua ya pamba, wadudu wachanga hupenya ndani na kuwa vigumu kuwadhibiti kwa viuadudu.

“Hali hiyo inasababisha hasara kwa wakulima kwa kuwa inawalazimu kunyunyizia dawa mara nyingi, jambo ambalo pia ni hatari kiafya na linaweza kuathiri ubora wa pamba ya Tanzania kwenye soko la kimataifa,” anasema Dk Mkiga.
Kutokana na mwingiliano wa watu unaosababishwa na shughuli mbalimbali za kiuchumi katika mikoa yenye zuio la kulima pamba, kumekuwa na hamasa kubwa kwa wananchi kutaka kulima zao hilo.

TARI, kwa kushirikiana na Bodi ya Pamba Tanzania (TCB), inafanya juhudi na kutekeleza mkakati wa kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa zuio hilo na pia kuhimiza kilimo cha mazao mbadala.

Hivi karibuni, timu ya watafiti kutoka vituo vya TARI Ukiruguru na Uyole ilitembelea Mkoa wa Mbeya kwa ajili ya majadiliano na wadau, wakiwemo viongozi wa serikali, vyama vya siasa, halmashauri na wakulima kuhusu mustakabali wa wakulima wa mikoa hiyo kutaka kujihusisha na kilimo cha pamba.

Mkurugenzi wa TARI Ukiruguru, Dk Paul Saidia anasema majadiliano yalilenga kujenga uelewa wa pamoja kuhusu zuio la pamba na kushawishi wakulima kuangazia mazao mbadala. “Viongozi wa maeneo haya wana nafasi muhimu sana kuhakikisha wakulima wanaelewa sababu za zuio hili na kutafuta mbadala wa pamba kama alizeti, ufuta, mpunga na karanga,” anasema Dk Saidia.

Viongozi wa Mkoa wa Mbeya wanaunga mkono juhudi hizi wakisisitiza umuhimu wa utafiti wa kina kubaini kama inawezekana kudhibiti mdudu huyo kwa njia rafiki kwa mazingira. Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa
wa Mbeya, Lengaeli Akyoo anasisitiza umuhimu wa elimu kwa wadau kuelewa hatari ya funza huyo.

“Tutaendelea kutoa elimu kwa wadau ili kuelewa hatari za funza mwekundu. Ni muhimu wakulima waelimishwe pia kuhusu mazao mbadala ili wasikose fursa za kipato,” anasema.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Kanali Maulid Surumbu anasisitiza maofisa ugani kuwa karibu na wakulima kuhakikisha kilimo cha mazao mbadala kinafanyika kwa ufanisi. Diwani wa Kata ya Kambikatoto, Christopher Mchaphu aliwahi kulima pamba kabla ya zuio.

Anasema, “Awali, sikujua kuhusu funza mwekundu. Sasa nimeelewa athari zake. Tunaomba tuelimishwe zaidi kuhusu kilimo bora cha mazao mbadala na masoko yake.”

TARI inaendelea na utafiti wa kina kubaini ikolojia na baiolojia ya funza mwekundu, hasa kutokana na mabadiliko ya tabianchi. Matokeo ya utafiti huu yataiwezesha serikali kufanya uamuzi sahihi kutatua changamoto iliyopo na kujua hatma ya zuio kilimo cha pamba katika mikoa husika.

Kwa sasa TARI, TCB na wadau wengine wanaendelea kuhamasisha na kutoa elimu kuhusu zuio hilo huku wakihamasisha kilimo bora cha mazao mbadala kama ufuta, alizeti, mpunga, karanga na mengineyo mpaka tafiti za
kina kuhusu funza mwekundu na udhibiti wake zitakapo kamilika.

Zuio la kilimo cha pamba katika Nyanda za Juu Kusini si adhabu kwa wakulima, bali ni hatua ya kulinda zao hilo la biashara dhidi ya uharibifu wa funza mwekundu.

Ushirikiano kati ya serikali, wakulima na watafiti utasaidia kubaini njia bora ya kushughulikia changamoto hii bila
kuhatarisha afya, mazingira, na soko la pamba la Tanzania.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button