Mganga aliyekutwa akifuga fisi Jela miaka 20

Mahakama ya Wilaya Bariadi mkoani Simiyu imemhukumu kifungo cha miaka 20 jela pamoja na kuchapwa viboko 12 Emmanuel John (31) maarufu kama Chief wa Kilulu kwa kosa la kukutwa na nyara za serikali aina ya fisi akiwa hai akiishi naye nyumbani kwake.
Mshtakiwa huyo mkazi wa kijiji cha Kilulu kata ya Bunhamala wilayani humo na mganga wa kienyeji, amehukumiwa adhabu hiyo katika kesi namba 2458/2025 iliyokuwa inamkabili kwenye Mahakama hiyo.
Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo Caroline Kiliwa baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka.
Awali akisoma kosa la mshitakiwa Mwendesha Mashtaka kutoka Ofisi ya Mashtaka Mkoa, Lupiana Mahenge ameielezea Mahakama kuwa kosa la mtuhumiwa huyo ni kukutwa nyara ya serikali ambayo ni fisi akiwa hai akimfuga nyumbani kwake kinyume cha sheria.
Amesema Januari 01, 2025 katika eneo la kijiji cha Kilulu mtuhumiwa alikamatwa kufuatia Jeshi la Polisi kupata taarifa kutoka kwa raia wema kuhusu mtuhumiwa kuishi na fisi hai ndani kwake.



