Kampeni yazinduliwa kuimarisha uchumi wa buluu Afrika Mashariki

Ascending Africa imezindua kampeni inayolenga kurejesha na kuimarisha uchumi wa buluu kwa Afrika Mashariki.

Kampeni hiyo iitwayo ‘Kilindini’, inalenga kukuza usimamizi endelevu wa rasilimali za baharini, kusaidia jamii za pwani, na kupambana na shughuli haramu zinazotishia Bahari ya Hindi Kusini Magharibi.

Neno “Kilindini” limetokana na Kiswahili likimaanisha “kina kirefu” au “vilindini”, likiwa ishara ya urithi tajiri wa baharini wa ukanda huu, wenye mizizi katika utamaduni, biashara, na shughuli za kiuchumi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo jijini Nairobi hivi karibuni, msemaji wa Kampeni ya Kilindini, Bw Tendai Mtana, alisisitiza umuhimu wa kuchukua hatua za haraka.

“Uchumi wa buluu wa Afrika Mashariki una uwezo mkubwa ambao haujatumika ipasavyo kuendesha ukuaji wa uchumi, kuboresha maisha, na kuhifadhi viumbe wa baharini. Kupitia mpango huu, tunalenga kurejesha uwiano, kuwawezesha jamii za pwani, na kuhakikisha ustawi wa muda mrefu wa bahari inayotuhifadhi sote,” alisema Bw Mtana.

Kampeni hii inalenga kushughulikia changamoto zinazoathiri uendelevu wa rasilimali za Bahari ya Hindi.

Uvuvi haramu, usioripotiwa, na usiodhibitiwa (IUUF) unasababisha hasara ya zaidi ya dola milioni 415 kwa mwaka katika ukanda wa Bahari ya Hindi Kusini Magharibi, huku ukichangia kupungua kwa hifadhi ya samaki muhimu kwa jamii za pwani.

Uvuvi huo pia unachochea uhalifu kama usafirishaji haramu wa binadamu na magendo, hivyo kuongeza hatari za kiusalama baharini.

Uvuvi wa kupindukia na mabadiliko ya tabianchi vinapunguza idadi ya samaki kwa kiwango cha hatari, hivyo kuhatarisha usalama wa chakula na vyanzo vya kipato. Uchafuzi wa mazingira, kufa kwa matumbawe, na uharibifu wa makazi ya viumbe baharini kunadhoofisha mifumo ya ikolojia.

Ulinzi wa mikoko, miamba ya matumbawe, na nyasi baharini ni muhimu katika kudumisha bayoanuai.

Bahari ya Hindi Kusini Magharibi, ikiwa mojawapo ya njia kuu za kimataifa za usafirishaji wa mizigo, inakabiliwa na vitisho vinavyoongezeka vya uharamia, usafirishaji haramu, na uvuvi usiodhibitiwa, hali inayohatarisha maslahi ya kiuchumi ya kanda na dunia kwa ujumla.

Ili kukabiliana na changamoto hizi, Kampeni ya Kilindini inatekeleza mkakati madhubuti unaojumuisha kuweka viwango vya uvuvi, marufuku za msimu, na mipango ya uhifadhi ili kurejesha idadi ya samaki na kulinda riziki za wavuvi.

Pia, kampeni inalenga kutoa elimu na mafunzo kwa wakazi wa pwani ili kuwawezesha kushiriki katika uvuvi endelevu na juhudi za uhifadhi wa mazingira ya baharini.

Ushirikiano kati ya mataifa ya Afrika Mashariki utakuwa muhimu katika kushughulikia changamoto za pamoja za baharini kwa ufanisi. Aidha, kampeni hii itatumia teknolojia kama ufuatiliaji wa satelaiti, mifumo ya akili bandia (AI) kufuatilia uhamaji wa samaki, na matumizi ya droni ili kuongeza ufanisi wa doria na utekelezaji wa kanuni za uvuvi.

“Mustakabali wa uchumi wa buluu wa Afrika Mashariki si suala la kikanda pekee—ni kipaumbele cha kimataifa,” alisisitiza Mtana.

Aliwahimiza serikali, mashirika, na watu binafsi kuchukua hatua kwa kuwekeza katika teknolojia, kusaidia juhudi za uhifadhi zinazoongozwa na jamii, na kushinikiza sera madhubuti za baharini.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button