Tufuate maelekezo ya wataalamu kujikinga magonjwa ya milipuko

JUZI Wizara ya Afya ilitoa mwongozo kwa wasafiri kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa homa ya nyani kama ilivyotangazwa kuwepo kwa ugonjwa huo nchini.
Kwa mujibu wa wizara hiyo, mwongozo huo namba 16 utakuwa ukihuishwa mara kwa mara kadri itakavyohitajika, kutokana na ugonjwa huo kuwepo nchini baada ya hivi karibuni watu wawili kubainika kuugua ugonjwa huo.
Serikali imebainisha kuwa imeanza kutekeleza afua za afya ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo ndani na nje ya mipaka ya nchi kwa kuzingatia Kanuni za Afya za Kimataifa za Mwaka 2005.
Miongoni mwa hatua zilizoainishwa katika mwongozo huo ni wasafiri na wafanyakazi wote katika maeneo ya mipakani kutakiwa kuzingatia hatua za kuzuia na kudhibiti maambukizi kwa kunawa mikono, na kuacha angalau umbali wa meta moja baina ya mtu mmoja na mwingine.
Pia, kutoa taarifa kuhusu mtu yeyote mwenye dalili za ugonjwa kwa kupiga simu namba 199 bure, kutoa taarifa ofisi ya afya mipakani au kituo cha afya kilicho karibu.
Hatua nyingine ni katika maeneo yote ya mipaka yaani viwanja vya ndege, mipaka ya nchi kavu na bandari wasafiri wote watafanyiwa uchunguzi wa awali wa afya ikiwamo kupimwa joto la mwili na watakaobainika kuwa na homa na au vipele watafanyiwa uchunguzi wa kina wa kiafya.
Hatua hii ya serikali kutangaza mwongozo huu ni muhimu kwa sababu inawezesha wananchi kufahamu jinsi ya kukabiliana na ugonjwa huu na kuchukua hatua.
Tumeona jinsi serikali ilivyoshughulikia ugonjwa mwingine wa Marburg hivi karibuni na kufanikiwa kuudhibiti, hivyo tuna imani katika ugonjwa huo wa homa ya nyani pia itafanya hivyo kutokana na weledi wake katika kusimamia afya za Watanzania.
Kubwa na la msingi ni kwa wananchi wote kuchukua tahadhari zote zinazohitajika kuepuka kupata maambukizi ikiwamo kufuata mwongozo uliotolewa, pamoja na kufuatilia taarifa zitakazokuwa zinatolewa na serikali kwa kila hatua.
Kwa wasafiri na jamii kwa ujumla kubwa linalohitajika ni ushirikiano na vyombo vya serikali hasa kwa wasafiri na watu wengine ambao watahitajika kufanyiwa uchunguzi wa afya zao kwa kuhisiwa au kwa taratibu kwa kuwa wanatoka nje ya nchi.
Hii itasaidia katika udhibiti kwa sababu waswahili wanasema kinga ni bora kuliko tiba, hivyo ni muhimu kudhibiti hali hii kwa kuchukua hatua zote stahiki.
Sisi tunaamini magonjwa hayo ya milipuko yanadhibitiwa kama ambavyo tumeshuhudia katika magonjwa yaliyowahi kulipuka nchini, la msingi jamii ifuate kila maelekezo yanayotolewa na serikali kupitia wataalamu wake, na pia ijiepushe na taarifa zisizo rasmi kwani zinaweza kuwachanga na hivyo kutoa mwanya wa maambukizi zaidi.



