Dk Mwinyi: Tanzania imeheshimika mashindano ya Kurani

DAR ES SALAAM; RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema Tanzania imepata manufaa na heshima kwa kuandaa mashindano ya 25 ya kuhifadhi Kurani yaliyohusisha mabara yote duniani.
Dk Mwinyi alisema hayo wakati akihitimisha mashindano hayo yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam jana. Maelfu ya wananchi walihudhuria.
Alisema mashindano hayo yameidhihirishia dunia kwamba Tanzania ni nchi salama na inayoaminika kuendesha mashindano, makongamano na mikutano mikubwa ya kimataifa.
Dk Mwinyi alisema mashindano hayo yamekuwa kielelezo cha kuwepo kwa uhuru wa kuabudu uliomo ndani ya nchi na serikali yake kwa watu wake wote.
Alisema kufanyika kwa mashindano hayo ni ushahidi kuwa Tanzania inatoa ushirikiano sawa na wa kutosha kwa shughuli za kidini bila kujali tofauti za dini au madhehebu.
“Jambo hilo liliasisiwa na waasisi wetu na ni muhimu kwa sababu linajenga umoja, mshikamano wa kitaifa na linaenzi amani na utulivu wa nchi,” alisema Dk Mwinyi.
Alisema kwa kuwa mashindano hayo yamefanyika katikati ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni vema Waislamu wakazidisha usomaji wa kitabu kitakatifu cha Kurani kwa sababu kimeteremshwa ndani ya mwezi huo.
Dk Mwinyi aliishukuru taasisi ya Al Hikma na Mdhamini Mkuu wa mashindano Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) kwa kusimamia na kugharimia mashindano hayo.
Aliwakumbusha Waislamu wawapeleke watoto madrasa wajifunze kusoma kitabu hicho kwa sababu hiyo ni njia sahihi itakayozalisha mashehe na maulamaa wa baadaye.
Aidha, Dk Mwinyi aliwakumbusha Waislamu kutumia muda uliobaki ndani ya kumi la pili la Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kumuomba Mwenyezi Mungu msamaha kwa makosa waliyofanya kwa kujua na kutokujua.
Aliwasihi waumini wote wa Kiislamu kuhakikisha wanatoa misaada kwa wanaohitaji kwa sababu Mwenyezi Mungu anapenda zaidi watu wanaotumia uwezo wao kusaidia wengine.
Dk Mwinyi alizitaka taasisi za fedha nchini pamoja na wafanyabiashara kuunga mkono juhudi za Taasisi ya Al Hikma katika kuandaa mashindano ya Kurani ili taifa liweze kupata manufaa zaidi kimataifa.
Katika mashindano hayo, mshindi wa kwanza anatoka Urusi ambaye ni Aeimiddin Farkhuddin aliyepata alama 99.4 na kujipatia zawadi ya Dola za Marekani 11,150 sawa na Sh milioni 30 na medali ya dhahabu yenye thamani ya Sh milioni 2.8.
Mshindi wa pili ni Abdul Mohamed Jumaa kutoka Libya aliyepata alama 99.06 na kujipatia Dola za Marekani 7,450 sawa la Sh milioni 20.4 na medali ya fedha yenye thamani ya Sh milioni moja.
Mshindi wa tatu kwa mujibu wa jopo la majaji kutoka Uganda, Kuwait na Tanzania ni Islam Mahmoud kutoka Misri aliyepata alama 98.53 na kupata Dola za Marekani 4,400 sawa na Sh milioni 11.83 pamoja na medali ya fedha yenye thamani ya Sh milioni moja.
Matokeo hayo yalionesha kuwa mshindi wa nne anatoka Guyana katika Bara la Amerika ya Kusini ambaye ni Swalehe Mohamed Rahim aliyepata alama 98.4 na kujishindia kitita cha Dola 3,000 sawa na Sh milioni nane pamoja na medali ya fedha yenye thamani ya Sh milioni moja.
Aidha, Tanzania kupitia Kassim Ayoub Salim alishika nafasi ya tano kwa kupata alama 98.36 na kupata Dola za Marekani 2,000 sawa na Sh milioni 5.38 pamoja na medali ya fedha yenye thamani ya Sh milioni moja.



