Al Hikma kugharimia ndoa za vijana 200

DAR ES SALAAM; TAASISI ya Al Hikma imesema itagharimia ndoa za vijana 200 ili watimize maagizo ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Pia, taasisi hiyo imesema itawafanyia suna watoto 1,050 kutoka Tanzania ikiwa ni sehemu ya kutoa kwa jamii ya Watanzania.

Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Nurdin Kishki alisema hayo kwenye mashindano ya kuhifadhi Kurani tukufu yaliyoshirikisha vijana kutoka mabara sita duniani kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam jana.

Kishki alisema Rais wa taasisi hiyo, Sharif Abdulkadir ameridhia kati ya vijana 200 watakaolipiwa gharama za ndoa zao, 100 watatoka Tanzania na wengine 100 watatoka Burundi.

“Al Hikma itafanya suna kwa vijana 1,000 kutoka Tanzania na Kampuni ya Bima ya Poly Clinic imeongeza vijana 50 hivyo vijana 1,050 watafanyiwa suna kwa gharama zetu,” alisema.

Kishki alisema gharama zote za harusi na ndoa kwa vijana hao 200 zinajumuisha mahari, mavazi pamoja na chakula. Aliwataka vijana ambao hawajaoa kuchangamkia fursa hiyo ili kutimiza ndoto zao.

Mufti wa Tanzania, Shehe Abubakar Zuber Bin Ali alisema anajivunia mashindano hayo kwa sababu yanajenga undugu, umoja na mshikamano miongoni mwa Watanzania.

Alitoa wito kwa Watanzania kutokubali kuingia katika mitego ya wanasiasa wanaojali maslahi binafsi na kuharibu amani na utulivu wakati wa Uchaguzi Mkuu mwaka huu.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button